Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 79

Kwa Nini Kutakuwa na Uharibifu Wakati Ujao?

Kwa Nini Kutakuwa na Uharibifu Wakati Ujao?

LUKA 13:1-21

  • YESU AFUNDISHA SOMO KUTOKANA NA MISIBA MIWILI

  • MWANAMKE KILEMA APONYWA SIKU YA SABATO

Yesu ametumia njia nyingi ili kuwachochea watu wafikirie kuhusu uhusiano wao pamoja na Yehova. Anapata fursa nyingine baada ya kuzungumza na watu waliokuwa nje ya nyumba ya Farisayo.

Baadhi yao wanataja kuhusu msiba fulani. Wanataja kuhusu “Wagalilaya ambao Pilato [Gavana Mroma Pontio] alikuwa amechanganya damu yao na dhabihu zao.” (Luka 13:1) Wanamaanisha nini?

Labda Wagalilaya hao ndio waliouawa maelfu ya Wayahudi walipompinga Pilato alipotumia pesa kutoka kwenye hazina ya hekalu kujenga mfereji wa kuleta maji Yerusalemu. Inawezekana Pilato alipata pesa hizo kwa kushirikiana na wasimamizi wa hekalu. Huenda wale wanaosimulia kuhusu msiba huo wanafikiri kwamba Wagalilaya hao walipatwa na msiba huo kwa sababu walikuwa na hatia ya matendo maovu. Yesu hakubaliani nao.

Anauliza: “Je, mnafikiri Wagalilaya hao walikuwa watenda dhambi wabaya zaidi kuliko Wagalilaya wengine wote kwa sababu walipatwa na mambo hayo?” Jibu lake ni hapana. Lakini anatumia tukio hilo kuwaonya Wayahudi: “Msipotubu, nyote mtaangamizwa vivyo hivyo.” (Luka 13:2, 3) Kisha Yesu anataja msiba mwingine ambao huenda umetokea hivi karibuni na labda unahusiana na ujenzi wa mfereji huo, anauliza:

“Wale 18 walioangukiwa na mnara huko Siloamu wakafa, je, mnafikiri walikuwa na hatia kuliko watu wengine wote wanaoishi Yerusalemu?” (Luka 13:4) Huenda umati ukafikiri kwamba watu hao walikufa kwa sababu ya uovu wao. Lakini tena Yesu hakubaliani na jambo hilo. Anajua kwamba “wakati na matukio yasiyotarajiwa” hutukia na huenda ndicho kisababishi cha msiba huo pia. (Mhubiri 9:11) Hata hivyo, watu wanapaswa kujifunza kutokana na tukio hilo. Yesu anasema: “Msipotubu, ninyi pia mtaangamizwa kama wao.” (Luka 13:5) Lakini kwa nini anakazia somo hilo sasa?

Ni kwa sababu ya kipindi alichofikia katika huduma yake, naye anatoa mfano huu ili kufafanua jambo hilo: “Mtu fulani alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaenda kutafuta matunda kwenye mti huo lakini hakupata. Ndipo akamwambia mtunza-mizabibu, ‘Kwa miaka mitatu nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, lakini sijayapata. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’ Akamjibu, ‘Bwana, uache kwa mwaka mwingine mmoja niupalilie na kuutia mbolea. Ukizaa matunda wakati ujao, vema; la sivyo, utaukata.’”—Luka 13:6-9.

Kwa zaidi ya miaka mitatu, Yesu amekuwa akijitahidi kupanda imani miongoni mwa Wayahudi. Lakini, ni wachache ambao wamekuwa wanafunzi wake na wanaweza kuonwa kuwa matunda ya kazi yake. Sasa, katika mwaka wa nne wa huduma yake, anaongeza jitihada zake. Ni kana kwamba alikuwa akilima na kuweka mbolea kwenye mtini wa Wayahudi kwa kuhubiri na kufundisha huko Yudea na Perea. Amepata matokeo gani? Ni Wayahudi wachache tu wanaoitikia. Kwa ujumla, taifa hilo linakataa kutubu na sasa wanakabili uharibifu.

Mtazamo huo wa wengi kutokubali unaonekana tena muda mfupi baadaye katika siku ya Sabato. Yesu anafundisha katika sinagogi. Anamwona mwanamke ambaye anateswa na roho mwovu, na amejikunja kwa miaka 18. Kwa huruma, Yesu anamwambia: “Mwanamke, umefunguliwa kutoka kwa udhaifu wako.” (Luka 13:12) Yesu anaweka mikono juu yake, naye mwanamke huyo ananyooka papo hapo na kuanza kumtukuza Mungu.

Jambo hilo linamkasirisha msimamizi wa sinagogi, naye anasema hivi: “Kuna siku sita za kufanya kazi; basi, njooni mponywe katika siku hizo, bali si siku ya Sabato.” (Luka 13:14) Msimamizi huyo hakatai kwamba Yesu ana nguvu za kuponya, badala yake, anawashutumu watu kwa kuja kuponywa siku ya Sabato! Yesu anatoa jibu linalopatana na akili: “Wanafiki, je, kila mmoja wenu hamfungui ng’ombe au punda wake kutoka kwenye kibanda siku ya Sabato na kumpeleka akanywe maji? Je, haifai kwa mwanamke huyu, binti ya Abrahamu, ambaye Shetani alikuwa amemfunga kwa miaka 18 afunguliwe kutoka kwenye kifungo hicho siku ya Sabato?”—Luka 13:15, 16.

Wapinzani hao wanaaibika, lakini umati unashangilia kwa sababu ya mambo yenye utukufu wanayoona Yesu akifanya. Kisha Yesu akiwa Yudea anarudia mifano miwili ya kinabii kuhusu Ufalme, aliyokuwa amesimulia awali akiwa katika mashua kwenye Bahari ya Galilaya.—Mathayo 13:31-33; Luka 13:18-21.