Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Unatumia Teknolojia Kwa Busara?

Je, Unatumia Teknolojia Kwa Busara?

Jenni ni mraibu wa mchezo fulani wa video. Anasema hivi: “Mimi hutumia saa nane kwa siku kucheza mchezo huo, na hilo limekuwa tatizo kubwa.”

Dennis alijaribu kutotumia simu na Intaneti kwa siku saba. Alifanikiwa kufanya hivyo kwa saa 40 tu.

Jenni na Dennis si matineja. Jenni ana umri wa miaka 40 na ana watoto wanne. Dennis ana umri wa miaka 49.

JE, UNATUMIA teknolojia? * Wengi watajibu ndiyo, na wana sababu nzuri ya kujibu hivyo. Vifaa vya kielektroniki ni vya muhimu katika kazi, maisha na burudani.

Hata hivyo, kama vile Jenni na Dennis, watu wengi wanatumia teknolojia kupita kiasi. Kwa mfano, Nicole, mwenye umri wa miaka 20 anasema hivi: “Ninasikitika kusema kwamba ninaipenda sana simu yangu ya mkononi. Mimi huhakikisha kwamba haiko mbali nami. Ninapokuwa katika eneo ambalo hakuna mtandao, mimi huchanganyikiwa, na baada ya nusu saa tu kupita, nami hutazamia kwa hamu kutumia simu ili kuona ikiwa nimetumiwa ujumbe wowote. Ninajua jambo hilo linaweza kuonekana kuwa la kipuuzi!”

Wengine hutumia simu au vifaa vingine vya mawasiliano usiku mzima ili kusoma ujumbe au kuona ikiwa programu fulani imeboreshwa. Huenda wakahisi vibaya sana wanapojaribu kuacha kutumia teknolojia. Baadhi ya watafiti wanafafanua tabia hiyo kuwa uraibu, iwe unatokana na matumizi ya teknolojia, Intaneti au kifaa cha mkononi kama vile simu. Wengine wanasita kutumia neno “uraibu” na kuamua kufafanua tabia hiyo kuwa tatizo gumu, sugu, au kutojidhibiti.

Hata hali hiyo iwe imepewa jina gani, matumizi yasiyofaa ya teknolojia yanaweza kuwa na madhara. Katika visa fulani, teknolojia imetenganisha washiriki wa familia. Kwa mfano, msichana mwenye umri wa miaka 20 analalamika hivi: “Siku hizi baba yangu hajui kinachoendelea maishani mwangu. Yeye hukaa sebuleni na kuandika barua-pepe huku akiongea nami. Hawezi kuweka simu yake chini. Ni kweli kwamba ananijali, lakini pindi fulani sioni ikiwa kwa kweli anahisi hivyo.”

“Kuwasaidia Waraibu wa Teknolojia”

Ili kuwasaidia watu kutumia kwa busara teknolojia, China, Korea Kusini, Uingereza na Marekani, zimeanzisha vituo “vya kuwasaidia waraibu wa teknolojia,” ambamo mtu hutibiwa tatizo hilo kwa kuzuiwa kutumia Intaneti na vifaa vya mawasiliano kwa siku kadhaa. Kwa mfano, mfikirie Brett, kijana anayesema kwamba wakati fulani alikuwa akitumia saa 16 kwa siku kucheza michezo kwenye Intaneti. Anasema hivi: “Kila mara nilipoingia katika mtandao ni kana kwamba nilikuwa ninatumia dawa za kulevya.” Brett alipojiunga na kituo cha kuwasaidia waraibu wa teknolojia, tayari alikuwa amepoteza kazi, marafiki, na alikuwa mchafu kimwili. Unawezaje kuepuka hali hiyo mbaya?

CHUNGUZA MATUMIZI YAKO YA TEKNOLOJIA. Tafakari jinsi teknolojia inavyoathiri maisha yako. Jiulize maswali yafuatayo:

  • Je, mimi huudhika au hukasirika upesi nisipopata Intaneti au nisipotumia kifaa changu cha kielektroniki?

  • Je, mimi huendelea kutumia Intaneti au kifaa changu cha mkononi kupita wakati niliojiwekea?

  • Je, mimi hukosa kulala vizuri kwa sababu ya kuendelea kuangalia ujumbe katika simu au kifaa kingine cha mawasiliano?

  • Je, matumizi yangu ya teknolojia yananifanya nipuuze familia yangu? Je, washiriki wa familia yangu watakubaliana na jibu langu?

Ikiwa matumizi yako ya teknolojia yanafanya upuuze “mambo yaliyo ya maana zaidi,” yanayotia ndani familia yako na majukumu mengine, sasa ndio wakati wa kufanya mabadiliko. (Wafilipi 1:10) Jinsi gani?

JIFUNZE KUWEKA MIPAKA INAYOFAA. Kitu kizuri kinapotumiwa kupita kiasi kinaweza kudhuru mtu. Hivyo, iwe unatumia teknolojia kwa ajili ya kazi au burudani, weka kiwango hususa cha muda utakaotumia, na ushikamane na ratiba hiyo.

Dokezo: Kwa nini usiombe msaada kutoka kwa washiriki wa familia au rafiki zako? Biblia inasema: “Wawili ni afadhali kuliko mmoja, . . . kwa maana mmoja wao akianguka, yule mwingine anaweza kumwinua mwenzake.”—Mhubiri 4:9, 10.

Usikubali kuwa “mraibu”

Kadiri vifaa vipya vya mawasiliano vinavyofanya iwe rahisi zaidi kupata na kutumia habari, matumizi yasiyofaa ya teknolojia yatazidi kukua. Hata hivyo, usikubali kuwa “mraibu.” Kwa ‘kujinunulia wakati unaofaa,’ utaepuka kutumia vibaya teknolojia.—Waefeso 5:16.

^ fu. 5 Katika makala hii, neno “teknolojia” linarejelea vifaa vya elektroniki vinavyoweza kupata au kusambaza habari za kielektroniki kama vile barua-pepe, mawasiliano ya simu, ujumbe mfupi, video, muziki, michezo, na picha.