Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Naomba Penseli

Naomba Penseli

Naomba Penseli

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

HAIGHARIMU pesa nyingi, inaanza kufanya kazi mara moja, na haina uzito mkubwa. Inaweza kuwekwa mfukoni vizuri. Haitumii umeme, haivuji, na alama zake zinaweza kufutwa. Watoto huitumia wanapojifunza kuandika, wachoraji huitumia kuchora picha za kupendeza, na wengi wetu huitumia kuandika habari fupi-fupi. Naam, kifaa hicho chenye bei rahisi na kinachotumiwa sana ulimwenguni ni penseli. Penseli ilivumbuliwa bila kutarajiwa katika maeneo ya vijijini huko Uingereza. Acheni tuwasimulie jinsi ilivyogunduliwa na kutengenezwa.

Risasi Nyeusi

Katika karne ya 16, mabonge ya kitu fulani cheusi yaligunduliwa chini ya kilima cha Borrowdale, kwenye bonde la Wilaya ya Lake kaskazini mwa Uingereza. Ingawa madini hayo yalifanana na makaa ya mawe, hayangeweza kuungua; nayo yaliacha alama nyeusi inayong’aa iliyoweza kufutwa. Kwa kuwa kitu hicho kingebaki kwenye vidole mtu alipokigusa, watu walifunika mabonge ya kitu hicho kwa ngozi ya kondoo. Iwapo kilikuwa katika umbo dogo jembamba kilifungwa kwa kamba. Hakuna anayejua wazo la kufunika risasi nyeusi kwa mbao lilianza jinsi gani, lakini kufikia miaka ya 1560, penseli zilikuwa zimeingizwa bara la Ulaya.

Muda si muda risasi nyeusi ikawa ikichimbwa na kusafirishwa ili kutosheleza mahitaji ya wachoraji, na kwa ujumla katika karne ya 17, ilikuwa ikitumika kila mahali. Wakati huohuo watengenezaji wa penseli walijaribu mbinu mbalimbali kuiboresha ili kutokeza kifaa kizuri cha kuandikia. Kwa kuwa risasi ya Borrowdale ilikuwa safi na rahisi kuchimbuliwa, wezi na wafanyabiashara wa magendo walianza kuiiba. Kwa sababu hiyo, Bunge la Uingereza lilipitisha sheria mnamo 1752 la kuwaadhibu wezi wa risasi nyeusi kwa kuwafunga.

Mnamo 1779, mwanakemia Mswedi Carl W. Scheele alifanya ugunduzi wenye kushangaza kwamba risasi nyeusi haikuwa risasi bali ilikuwa aina laini ya kaboni safi. Miaka kumi baadaye mwanajiolojia Mjerumani Abraham G. Werner aliiita grafati, kutokana na neno la Kigiriki graphein, linalomaanisha “kuandika.” Naam, tofauti na zinavyoitwa, kalamu za risasi hazina risasi yoyote!

Maendeleo ya Kutengeneza Penseli

Kwa miaka mingi grafati ya Uingereza ilitawala biashara ya penseli kwa kuwa ilikuwa safi na ingeweza kutumiwa mara tu baada ya kuchimbuliwa. Kwa kuwa grafati ya Ulaya ilikuwa ya hali ya chini, watengenezaji wa penseli walihitaji kuichanganya na vitu mbalimbali ili kuboresha risasi hiyo. Injinia Mfaransa Nicolas-Jacques Conté alichanganya grafati (kaboni) iliyosagwa na udongo wa mfinyanzi, akafanyiza vitu kama maumbo ya vijiti, na kuvichoma katika tanuru. Kwa kubadili kiasi cha mchanganyiko wa grafati na udongo wa mfinyanzi, alifaulu kutengeneza penseli zenye rangi nyeusi inayotofautiana. Mbinu hiyo bado inaendelea kutumika. Conté aliuandikisha kisheria ugunduzi wake mnamo 1795.

Katika karne ya 19, utengenezaji wa penseli ukaja kuwa biashara kubwa. Grafati ilivumbuliwa katika sehemu kadhaa kutia ndani Siberia, Ujerumani, na ile inayojulikana sasa kama Jamhuri ya Cheki. Viwanda vilianzishwa katika sehemu mbalimbali za Ujerumani na kisha Marekani. Kubuniwa kwa mashine na utengenezaji wa penseli kwa wingi ulisababisha bei ya penseli kushuka, na kufikia karne ya 20 hata mtoto wa shule alitumia penseli.

Penseli Leo

Kukiwa na mamia ya mabilioni ya watengenezaji ulimwenguni pote, penseli imekuwa kifaa cha hali ya juu cha kuandikia na kuchorea. Penseli ya kawaida inaweza kuchora mstari wenye urefu wa kilomita 56 na kuandika maneno 45,000. Pia kuna penseli za kipekee ambazo risasi zake ni nyembamba sana hivi kwamba hazihitaji kuchongwa. Badala ya kutengezwa kwa grafati, kuna penseli nyingine ambazo zimetengenezwa kwa rangi mbalimbali.

Penseli ina matumizi mengi na inafanya kazi vizuri. Haionekani kwamba siku moja haitatumiwa. Kwa hiyo kwa miaka mingi ijayo, ukiwa nyumbani au kazini, bado utasikia mtu akisema, “Naomba penseli.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]

RISASI INAINGIZWAJE KWENYE PENSELI?

Mchanganyiko wa grafati iliyosagwa, udongo wa mfinyanzi, na maji unaingizwa ndani ya mfereji mdogo wa bati na unatokea upande wa pili ukifanana na tambi ndefu. Baada ya kukaushwa, kukatwa, na kuchomwa kwenye tanuru, risasi hiyo inatumbukizwa ndani ya mafuta ya moto na nta. Mbao, hasa za mwerezi ambazo zinaweza kuchongwa kwa urahisi, zinapasuliwa pande mbili zinazolingana na unene wa penseli. Hayo hufanywa baada ya mbao hizo kupigwa randa na kuchonga mfereji mwembamba. Risasi zinaingizwa kwenye mifereji katika upande mmoja wa mbao, na ule upande mwingine unabandikwa kwa gundi na kugandamizwa juu ya sehemu ile nyingine. Gundi inapokauka penseli hukatwa vipande-vipande. Baada ya kuwekwa katika umbo fulani, kupigwa msasa, kupakwa rangi na kuwekwa nembo ya mtengenezaji na maelezo mengine, sasa penseli inakuwa tayari kutumiwa. Wakati mwingine kifutio huwekwa sehemu ya mwisho ya penseli.

[Hisani]

Faber-Castell AG

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]

NITUMIE PENSELI GANI?

Ili kuchagua penseli inayofaa, unahitaji kutazama herufi au namba zilizoandikwa katika penseli hiyo. Alama hizo huonyesha kiwango cha ugumu au ulaini wa risasi. Risasi laini huacha alama nyeusi zaidi.

Penseli yenye alama HB ni ya daraja la kati na ina matumizi mengi.

Alama B inawakilisha risasi laini. Nambari kama vile 2B au 6B zinaonyesha kiwango cha ulaini—kadiri namba inavyokuwa kubwa, ndivyo risasi inavyozidi kuwa laini.

Alama H inawakilisha risasi ngumu. Kadiri namba inavyokuwa kubwa—2H, 4H, 6H, ndivyo risasi inavyozidi kuwa ngumu.

Alama F inawakilisha penseli yenye ncha kali.

Nchi nyingine zinatumia mfumo tofauti. Kwa, mfano nchini Marekani penseli namba 2 inalingana na HB. Katika mfumo huo, kadiri namba inavyokuwa kubwa ndivyo risasi inavyozidi kuwa ngumu.