Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Manyoya—Ubuni wa Ajabu

Manyoya—Ubuni wa Ajabu

Manyoya—Ubuni wa Ajabu

KORONGO anapiga mabawa yake chini na kuruka juu. Kisha yeye huanza kujipinda-pinda akipaa bila juhudi yoyote kwa kusukumwa na upepo. Akibadili kidogo mwelekeo wa mabawa na mkia, ndege huyo huelea bila kupiga mabawa yake. Ni nini humwezesha kufanya hivyo kwa uwezo wa ajabu na kwa njia yenye kuvutia? Kinachomwezesha kufanya hivyo hasa ni manyoya yake.

Hakuna mnyama mwingine leo aliye na manyoya kama ya ndege. Ndege wengi wana manyoya ya aina tofauti-tofauti. Manyoya yanayoonekana kwa urahisi ni yale ya nje ambayo humfanya ndege awe na umbo laini linalomwezesha kupaa. Manyoya hayo yanatia ndani yale ya mabawa na ya mkia, yanayomwezesha ndege kuruka. Ndege mvumaji anaweza kuwa na manyoya ya nje 1,000 hivi, naye bata-maji zaidi ya 25,000.

Manyoya yamebuniwa kwa njia ya ajabu. Mhimili wa kati wa manyoya ambao unaitwa rachis unaweza kupindwa lakini ni imara sana. Vishina vya manyoya huota pande zote mbili za mhimili navyo kwa ujumla hutengeneza unyoya laini. Vishina hivyo huunganishwa kwa vitu vidogo vinavyoitwa barbule, na kufanyiza kitu kama zipu. Ndege huunganisha sehemu hizo ndogo za manyoya yao wanapojisafisha. Wewe unaweza kufanya hivyo pia kwa kuvuta unyoya kati ya vidole vyako.

Pande mbili za manyoya ambayo hasa hutumiwa kwa kuruka hazilingani, yaani, upande wa mbele wa unyoya ni mwembamba kuliko upande wa nyuma. Muundo huo wa ajabu unafanya kila unyoya uwe kama bawa dogo. Pia ukiangalia chini ya mhimili utaona mfereji. Mfereji huo unasaidia mhimili uweze kujipinda bila kuvunjika.

Manyoya Yana Matumizi Mengi

Katikati ya manyoya yanayoonekana kwa urahisi ya ndege wengi kuna manyoya membamba na marefu yanayoitwa filoplume na mengine yanayoitwa powder. Inasemekana kwamba kwenye miisho ya filoplume kuna vitu ambavyo husaidia ndege kutambua ikiwa kuna tatizo lolote kwenye manyoya ya nje, na hata vinaweza kusaidia kupima mwendo wake. Vishina vya manyoya ya powder vinavunjika na kutokeza unga-unga laini unaofikiriwa kuzuia maji. Ni manyoya hayo tu ambayo hukua kwa kuendelea na hayanyonyoki.

Zaidi ya kuwa na matumizi mengine, manyoya humkinga ndege kutokana na joto, baridi, na miale ya jua. Kwa mfano, bata wa baharini hawaonekani kama wanaathiriwa na pepo kali za baridi za baharini. Jinsi gani? Chini ya manyoya ya nje, kuna manyoya mengine mengi ya ndani yaliyo laini, yanayofanyiza tabaka la sentimita 1.7 na yanafunika sehemu kubwa ya mwili wa bata huyo. Manyoya hayo yana uwezo mkubwa wa kuhifadhi joto kuliko kifaa chochote kilichowahi kuundwa.

Manyoya huchakaa, kwa hiyo ndege huyanyonyoa manyoya yaliyozeeka na kutokeza mapya. Ndege wengi hunyonyoa manyoya ya mabawa na mkia kwa kutumia mpangilio fulani, kwa hiyo wao hudumisha uwezo wao wa kuruka.

“Yameundwa Bila Kasoro”

Ndege zinazoendeshwa na wanadamu zinahitaji ubuni wa hali ya juu. Vipi kuhusu ndege na manyoya? Kwa sababu hakuna uthibitisho wa mabaki ya kale ya wanyama, kuna ubishi mkali kati ya wanamageuzi kuhusu jinsi manyoya yalivyotokea. Gazeti Science News linasema kwamba kunapokuwa na mjadala kuhusu jambo hilo, wataalamu ‘husisimka na kufokeana sana.’ Mwanamageuzi mmoja aliyepanga mjadala kuhusu mageuzi ya manyoya, alikiri: “Sikuwahi kufikiri kwamba jambo lolote la kisayansi lingesababisha hali ya kutojidhibiti na chuki nyingi hivyo.” Ikiwa manyoya yalitokana na mageuzi, kwa nini mjadala mkali kama huo uzuke?

Kitabu kilichoandikwa kuhusu ndege (Manual of Ornithology—Avian Structure and Function) cha Chuo kikuu cha Yale kinasema hivi: “Tatizo ni kwamba manyoya hayana kasoro yoyote.” Manyoya hayajawahi kuhitaji marekebisho. Kwa kweli, “mabaki ya kale zaidi ya manyoya yanafanana kabisa na manyoya ya ndege wa leo.” * Hata hivyo, nadharia ya mageuzi inafundisha kwamba manyoya hutokezwa kutokana na mabadiliko ya polepole ya ngozi ya nje. Isitoshe, kitabu hicho kinaendelea kusema kwamba “manyoya hayawezi kuwa yalitokana na mageuzi bila kuwa na hatua za kuunganisha kipindi kimoja cha mageuzi na kingine.”

Kwa ufupi, hata wanasayansi hawawezi kubuni nadharia inayoweza kuonyesha jinsi mageuzi yalivyotokeza manyoya, isipokuwa tu kila hatua katika mabadiliko mengi yaliyorithiwa yasiyo na mpangilio yangeboresha sana uwezekano wa ndege kuokoka. Hata wanamageuzi wengi wanaona haiwezekani kwa mageuzi kutokeza kitu tata na kinachofanya kazi bila kasoro yoyote kama manyoya.

Zaidi ya hayo, ikiwa manyoya yangebadilika na kuwa bora baada ya muda mrefu, mabaki yaliyochimbuliwa ya wanyama wa kale yangeonyesha jinsi manyoya hayo yalivyokuwa awali. Lakini ni manyoya kamili tu ambayo yamewahi kupatikana. Kitabu hicho kuhusu ndege cha Chuo kikuu cha Yale kinasema hivi: “Nadharia ya mageuzi inapungukiwa kwa kuwa manyoya ni tata sana.”

Ndege Hawahitaji Manyoya Tu Ili Waruke

Wanamageuzi wana tatizo kubwa zaidi kuliko kueleza jinsi manyoya yalivyobuniwa kwa sababu sehemu zote za ndege zimebuniwa ili kumsaidia kuruka. Kwa mfano, ndege ana mifupa myepesi, iliyo wazi katikati, mfumo wa kupitisha hewa wenye uwezo wa ajabu, na misuli ya kipekee ya kumwezesha kupiga mabawa na kuyadhibiti. Vilevile ndege wana misuli kadhaa ya kuamua mahali kila unyoya unapopaswa kuwa. Na ndege wana neva za kuunganisha kila msuli na ubongo wao mdogo lakini wenye kushangaza ambao umeratibiwa kudhibiti mifumo yote hiyo kwa upatano na kwa usahihi wa hali ya juu. Naam, mifumo yote hiyo inahitajika ili ndege aruke, si manyoya peke yake.

Kumbuka kwamba kila ndege ametokana na chembe ndogo sana ambayo ina maagizo yote yanayohitajiwa ili akue na aongozwe na silika ili kwamba siku moja aweze kuruka. Je, mambo yote hayo yanaweza kutokea tu yenyewe? Au je, ule ufafanuzi rahisi zaidi kwamba ndege na manyoya yake yalitokana na Mbuni mwenye akili, ndio ufafanuzi unaopatana na akili na sayansi? Uthibitisho unajibu swali hilo.—Waroma 1:20.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Manyoya ya kale yaliyotajwa yalitoka kwa mnyama aliyetoweka aitwaye archaeopteryx ambaye mara nyingine husemwa kuwa “kiunganishi” katika mageuzi ya ndege. Hata hivyo, wanasayansi wengi hawakubali kwamba mnyama huyo anaonyesha mageuzi ya ndege.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

“UTHIBITISHO” WA UWONGO

Imegunduliwa kwamba uthibitisho fulani wa mabaki ya wanyama wa kale uliosemekana kuwa unathibitisha ndege walitokana na viumbe wengine ni wa uwongo. Kwa mfano, mnamo 1999, gazeti National Geographic lilikuwa na makala kuhusu mabaki ya kiumbe chenye manyoya na mkia kama wa dinosa. Gazeti hilo lilisema kwamba kiumbe hicho ni “kiunganishi halisi kilichokosekana katika mfuatano tata unaounganisha dinosa na ndege.” Hata hivyo, mabaki hayo yalisemekana kuwa ya uwongo kwani yalikuwa ya wanyama wawili tofauti. Kwa kweli, “kiunganishi halisi” kama hicho hakijawahi kupatikana.

[Hisani]

O. Louis Mazzatenta/National Geographic Image Collection

[Sanduku katika ukurasa wa 25]

UWEZO WA KUONA WA NDEGE

Rangi za manyoya ya ndege huwapendeza sana wanadamu. Lakini inawezekana kwamba manyoya yanawapendeza ndege hata zaidi. Ndege wengine wana aina nne za chembe za kuwawezesha kutambua rangi, huku wanadamu wana aina tatu tu. Uwezo huo wa ziada huwasaidia ndege kuona miale ambayo wanadamu hawawezi kuona. Wanadamu huona kwamba ndege wa kiume na wa kike wa jamii fulani wanafanana, lakini manyoya ya ndege wa kiume hutokeza miale hiyo kwa njia tofauti na ya ndege wa kike. Ndege wanaweza kuona tofauti hiyo, na hilo linaweza kuwasaidia kutambua wenzi.

[Picha katika ukurasa wa 23]

 

Vishina

Barbule

Rachis

[Picha katika ukurasa wa 24]

Manyoya ya “contour”

[Picha katika ukurasa wa 24]

Manyoya ya “filoplume”

[Picha katika ukurasa wa 25]

Manyoya ya “powder”

[Picha katika ukurasa wa 25]

Manyoya ya ndani

[Picha katika ukurasa wa 25]

Membe