Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 NCHI NA WATU | EL SALVADOR

Kutembelea El Salvador

Kutembelea El Salvador

MIAKA 500 hivi iliyopita, Wahispania walipofika katika nchi ambayo sasa inaitwa El Salvador, kabila kubwa la huko liliita eneo hilo Cuscatlán—jina linalomaanisha “Nchi ya Vito.” Leo, watu wengi nchini El Salvador ni wazao wa makabila ya wenyeji na Wazungu waliohamia huko.

Wenyeji wa El Salvador wanajulikana kuwa watu wenye bidii na urafiki. Ni wenye adabu na heshima. Watu husalimiana kwa adabu kabla ya kuanza mazungumzo au wanapoingia dukani kwa kusema, “Buenos días” (habari ya asubuhi) au “Buenas tardes” (habari ya alasiri). Kwa wenyeji wa El Salvador wanaoishi vijijini na katika miji midogo, wanaona ni utovu wa adabu kumpita mtu bila kumsalimu.

Kilimo cha kahawa kimebadili sana maisha ya watu wa El Salvador

Chakula wanachopenda sana ni pupusa,​—yaani, chapati ndogo zilizotengenezwa kwa unga wa mahindi (au mchele) na kisha kujazwa jibini, maharagwe, nyama ya nguruwe, au mchanganyiko mwingine. Mara nyingi pupusa huliwa kwa mchuzi wa nyanya na curtido, yaani, mchanganyiko wa kabeji, karoti, vitunguu, na siki yenye vikolezo. Ingawa watu fulani hula chakula hicho kwa kisu na uma, wenyeji hula kwa mikono.

Pupusa ni moja kati ya vyakula vinavyopendwa sana nchini El Salvador

 

Maporomoko ya Maji ya Los Tercios huko Suchitoto

 JE, WAJUA? El Salvador inaitwa nchi ya volkano. Kuna zaidi ya milima 20 ya volkano, na baadhi ya milima hiyo bado hulipuka. Maporomoko ya maji ya Los Tercios hutiririka juu ya safu ndefu za miamba iliyochongoka ambayo ilitokezwa na mlipuko wa volkano.

Kuna Mashahidi wa Yehova zaidi ya 38,000 nchini El Salvador, nao hukutana katika makutaniko 700 hivi. Wao huwafundisha watu 43,000 hivi Biblia katika lugha ya Kihispania, Kiingereza, na Lugha ya Ishara ya El Salvador.