Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ng’ombe Mwenye Manyoya Mengi

Ng’ombe Mwenye Manyoya Mengi

KWA sababu ya pembe ndefu zilizojipinda, manyoya marefu yanayoning’inia juu ya macho, na manyoya yanayofunika mwili wake imara, ng’ombe huyo wa sehemu za milimani hutambulika kwa urahisi.

Aina hiyo ya ng’ombe mwenye nguvu wa sehemu za milimani—ambaye ni mojawapo ya aina za kale zaidi za ng’ombe—amestahimili kwa karne nyingi hali mbaya ya hewa iliyopo katika maeneo ya milimani na katika visiwa vya Scotland. Hapo awali, ng’ombe ambao walilisha kwenye maeneo ya mbali ya milimani walikuwa wakubwa zaidi na wenye manyoya mekundu, lakini wale wa visiwa vilivyokuwa katika pwani ya magharibi walikuwa wadogo na kwa kawaida walikuwa na manyoya meusi. Leo, watu huona kwamba ng’ombe hao wa milimani ni jamii moja tu, na wanaweza kuwa na rangi nyekundu, nyeusi, kahawia, na manjano au hata rangi inayokaribia kuwa nyeupe.

Manyoya mengi ya ajabu-ajabu yanayoning’inia kwenye uso wa ng’ombe huyo yanatimiza fungu muhimu. Wakati wa majira ya baridi kali manyoya hayo humsaidia kujikinga dhidi ya upepo mkali, mvua, na hata theluji. Wakati wa majira ya kiangazi manyoya hayo humkinga dhidi ya wadudu wanaoruka ambao wanaweza kueneza magonjwa.

Katika Kiingereza, ng’ombe hao wanapokuwa katika kikundi wanarejelewa kuwa zizi. Neno hilo lilibuniwa nyakati za zamani, kwani wakati wa usiku wafugaji walikusanya ng’ombe wote katika mazizi yaliyokodiwa yaliyojengwa kwa mawe juu mlimani. Walifanya hivyo ili kuwalinda dhidi ya hali mbaya ya hewa na mbwa-mwitu.

Manyoya Yanayostaajabisha

Tofauti na ng’ombe wengine, ng’ombe hao wa milimani huwa na matabaka mawili ya manyoya. Tabaka la nje huwa na manyoya marefu yanayoweza kufikia urefu wa sentimita 33. Manyoya hayo humkinga dhidi ya mvua na theluji. Chini ya tabaka hilo, kuna manyoya laini, ambayo humsaidia kupata joto.

Jim, ambaye amefanya kazi ya kuwatunza ng’ombe hao kwa miaka mingi, anaeleza hivi: “Kuwaosha ng’ombe hawa kwa sabuni ni kazi ngumu, kwa sababu ni vigumu sana kwa manyoya yao kulowa maji!” Kwa sababu ya kufunikwa na manyoya mengi, ng’ombe hao wanaweza kustahimili mazingira magumu ya milimani yenye mvua na upepo wenye baridi kali, ambapo aina nyingine za ng’ombe haziwezi kustahimili.

Wakati wa kiangazi kunapokuwa na joto jingi na ukame, tabaka la juu la manyoya ya ng’ombe huyo hunyonyoka. Baadaye, wakati wa majira ya baridi kali tabaka jipya la manyoya hukua.

Mnyama Mwenye Thamani

Ingawa kondoo huharibu mimea kwa kutafuna mizizi na miche, ng’ombe​—kutia ndani ng’ombe hawa wa sehemu za milimani—​hawafanyi hivyo. Kwa kweli, ng’ombe hao wa sehemu za milimani huboresha maeneo ya malisho yasiyo na rutuba. Jinsi gani? Kwa kutumia pembe zake ndefu zenye nguvu na mdomo wake mpana, ng’ombe huyo huondoa vichaka ambavyo ng’ombe wa aina nyingine hawawezi kula. Kitendo hicho husaidia sana nyasi na miti kuanza kuchipuka tena.

Tabaka mbili za manyoya ya ng’ombe huyo huwa na manufaa mengine. Kwa sababu ng’ombe huyo hahitaji kuwa na mafuta mengi mwilini ili kudumisha joto, nyama ya ng’ombe huyo huwa na mafuta kidogo na protini nyingi na madini ya chuma kuliko nyama kutoka kwa ng’ombe wa aina nyingine. Aina hiyo bora ya nyama hupatikana bila kutumia gharama kubwa katika kumlisha ng’ombe huyo!

Tahadhari!

Ng’ombe hao wa sehemu za milimani wameishi karibu na wanadamu kwa muda mrefu. Wenyeji wa mapema wa Scotland waliwafuga ng’ombe wao kwenye orofa ya chini ya nyumba zao. Lengo lao likiwa ni kuongeza joto kwenye sehemu za juu za nyumba, ambako familia iliishi.

Ingawa kwa ujumla ng’ombe wa kufugwa ni watulivu, nyakati nyingine baadhi ya ng’ombe wa milimani wanaweza kuwa hatari. Kwa mfano, ng’ombe anayenyonyesha humlinda sana ndama wake. Pia, mtu anahitaji kuepuka kupita katikati ya kundi la ng’ombe hao na badala yake anapaswa kupita kando.

Uwezo wa ng’ombe hao wa kustahimili hali tofauti-tofauti za hewa kumewafanya waweze kuishi sehemu nyingi ulimwenguni. Wanapatikana sehemu za mbali upande wa kaskazini kama vile Alaska na nchi za Skandinavia, na wanaweza kupatikana wakilisha kwenye sehemu za juu sana zinazofikia kimo cha mita 3,000 kwenye Milima ya Andes. Wakati huohuo, ng’ombe hao wanaweza kuishi vizuri kwenye maeneo ya joto.

Nchi ya Scotland si maarufu tu kwa nguo zinazotengenezwa kutokana na manyoya, sketi za kukunjwa, na zumari aina ya bagpipes, lakini pia kwa sababu ya aina hii ya ng’ombe mwenye kupendeza wa sehemu za milimani. Je, mahali unapoishi kuna ng’ombe mwenye tabaka mbili za manyoya?