Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Tangu mwaka wa 2004, mara ambazo neno porn’ (ponografia) limetumiwa kwenye Intaneti ili kutafuta habari kupitia Google zimeongezeka mara tatu.”​—THE ECONOMIST, UINGEREZA.

“Mwanamke [Mrusi] anapoolewa, . . . kuna uwezekano wa asilimia 60 kwamba mume wake atampiga, au huenda ugomvi wao ukahusisha mwanamke huyo kupigwa.”​—MOSKOVSKIYE NOVOSTI, URUSI.

“Mwanasayansi au daktari mmoja kati ya saba nchini Uingereza ameshuhudia wenzake wakibadilisha kimakusudi au kuandika taarifa za uwongo wakati wa utafiti au wakati wa kuchapisha kitabu.”​—BRITISH MEDICAL JOURNAL, UINGEREZA.

“Idadi ya watu wanaopona kutokana na ugonjwa wa kansa nchini Marekani imeongezeka mara nne tangu mwaka wa 1971 kufikia karibu watu milioni 12 . . . Kwa sehemu kubwa idadi hiyo imetokana na ugonjwa huo kugunduliwa mapema kupitia uchunguzi wa kina, matibabu bora, na kuendelea kufanyiwa uchunguzi hata baada ya kupona.”​—UC BERKELEY WELLNESS LETTER, MAREKANI.

Muda mfupi kabla ya sherehe za Krismasi za mwaka wa 2011, mapigano yalizuka miongoni mwa makasisi na watawa 100 hivi wa madhehebu tofauti katika Kanisa la Uzaliwa wa Kristo, huko Bethlehemu. “Hilo ni jambo dogo sana ambalo . . . hutokea kila mwaka,” akasema kamanda wa polisi. “Hakuna aliyekamatwa kutokana na tukio hilo kwa sababu wote waliohusika ni watu wa Mungu.”​—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, MAREKANI.

Ukuta Mkubwa wa Kijani wa Afrika

Katika mwaka wa 2007, Muungano wa Afrika (AU) ulizindua mradi uliohusisha nchi zote za Afrika ukiwa na lengo la kuzuia kuenea kwa Jangwa la Sahara kwa kupanda miti. Nchi 11 zinapanda miche inayofaa katika eneo lenye urefu wa kilomita 7,600 na upana wa kilomita 15 kuanzia nchini Senegal upande wa Magharibi hadi nchini Djibouti upande wa Mashariki. “Tunahitaji kupanda miti ambayo watu hawatatamani kuikata kwa ajili ya mbao,” anasema Aliou Guissé, profesa wa ekolojia ya mimea katika Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop jijini Dakar, Senegal. Inatumainiwa kwamba maeneo hayo yatakayokuwa yamepandwa miti yatakuwa ni hifadhi ya mazingira na hivyo kutokeza rasilimali endelevu kwa jamii zinazozunguka.

Kwa Nini Wanadamu Hupiga Mwayo?

Wanasayansi hawana uhakika kwa nini wanadamu hupiga mwayo​—na wengine hata hupiga miayo mara kadhaa kwa siku. Hata watoto walio bado tumboni hupiga mwayo. Viumbe wengine pia hupiga mwayo kama vile nungunungu, mbuni, nyoka, na samaki. Kuna nadharia nyingi, zinazopingana, ambazo zimetolewa, lakini hakuna inayowaridhisha watafiti. Wanasayansi wengi wamesema kwamba kitendo hicho ambacho kwa kawaida hudumu sekunde sita hivi, huongeza oksijeni kwenye ubongo. Hata hivyo “kufikia sasa, watafiti hawajapata ushahidi unaoweza kuunga mkono wazo hilo,” linasema gazeti Science News. Uchunguzi mpya waliofanyiwa panya unaonyesha kwamba “huenda kupiga mwayo husaidia kupunguza joto kwenye ubongo.” Lakini hakuna aliye na jibu hakika.