Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wakati Jua Halichomozi

Wakati Jua Halichomozi

Wakati Jua Halichomozi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND

“JUA hutoka, jua hutua; huenda zake lirudie mahali litakapotokea tena,” inasema Biblia. (Mhubiri 1:5, Verbum Bible) Lakini kuanzia katikati ya Novemba hadi mwisho wa Januari, huenda kukawa na mabadiliko katika macheo na machweo katika maeneo mengi kaskazini mwa Mzingo wa Aktiki. Katika maeneo hayo inawabidi watu wavumilie usiku mrefu wa Aktiki katika majira ya baridi kali.

Kwa kiwango kidogo, maeneo yaliyo kusini mwa Mzingo wa Aktiki yanakuwa na usiku mrefu pia. Kwa mfano, mwangaza wa jua huonekana tu kwa saa sita hivi katika majira ya baridi kali huko St. Petersburg, Urusi; Helsinki, Finland; Stockholm, Sweden; na Oslo, Norway, majiji yaliyo umbali wa kilomita 800 hivi kusini mwa Mzingo wa Aktiki.

“Wazo la kwamba majira ya baridi kali katika maeneo ya Aktiki huwa na giza tititi si kweli,” anasema Ari, aliyelelewa huko Kiruna, Lapland ya Sweden. Sehemu kubwa ya siku inaweza kulinganishwa na machweo. Paula, msanii anayeishi kwenye Lapland ya Finland, anasema, “Wakati Lapland imefunikwa kwa theluji, rangi hugeuka na kuwa bluu na zambarau.”

Watu fulani huathiriwa na giza la majira ya baridi kali. “Ninaathiriwa sana na mabadiliko ya majira na hali ya hewa,” akaandika Jean Sibelius, mtungaji maarufu kutoka Finland. Aliongezea hivi: “Katika majira ya baridi kali, wakati mchana ni mfupi, mimi hufadhaika.” Mbali na Sibelius, watu wengine pia wamefadhaishwa na giza la majira ya baridi kali. Hata mwanafizikia Mgiriki Hipokrati (mnamo 460-377 K.W.K.) aliamini kwamba majira huathiri hisia za watu.

Hata hivyo, kufikia miaka ya 1980 ndipo mfadhaiko unaotokea wakati wa majira ya baridi kali ulipofafanuliwa kuwa ugonjwa. Uchunguzi umeonyesha kwamba asilimia ndogo kati ya watu wanaoishi katika maeneo yanayoathiriwa na majira hayo wanaugua ugonjwa wa majira ya baridi kali (SAD). Watu wengi zaidi wanaathiriwa na aina fulani ya ugonjwa huo ambayo si mbaya sana. Inaaminiwa kwamba mamia ya maelfu ya watu wanaathiriwa kwa kiwango fulani.

Andrei, anayeishi huko St. Petersburg, Urusi, anasema, “Ninahisi usingizi kila wakati.” Annika, anayeishi Finland, anahuzunika majira ya baridi kali yanapokaribia. “Wakati mwingine,” anasema, “giza hunifanya niwe na wasiwasi mwingi kana kwamba nimefungiwa katika sehemu isiyo na nafasi kubwa bila njia ya kutokea.”

Wataalamu wanapendekeza njia mbalimbali za kukabiliana na mfadhaiko unaotokea wakati wa majira ya baridi kali. Kwa mfano, baadhi yao hupendekeza kwamba mtu anapaswa kukaa nje kwa kipindi kirefu iwezekanavyo kunapokuwa na mwangaza wa jua. Wale wanaofanya kazi nje wakati wa mchana wanasema kwamba hawaathiriwi na mfadhaiko unaotokea wakati wa majira ya baridi kali.

Jarmo, ambaye amekabiliana na majira ya baridi ya baridi kali kaskazini na kusini mwa Finland anasema, “Kunapokuwa na giza zaidi, tunatumia mishumaa mingi zaidi na kuwasha taa nyingi zaidi.” Baadhi yao wamepata nafuu kwa kupata matibabu ya kumulikwa kwa mwangaza mwingi. Wengine huepuka giza linalotokea wakati wa majira ya baridi kali kwa kwenda likizo katika nchi zenye joto. Hata hivyo, wengine huonya kwamba baada ya watu kutoka likizo kwenye eneo kama hilo, huenda wafadhaike zaidi wanaporudi kwenye giza la majira ya baridi kali.

Ni muhimu pia kula vizuri. Kwa kuwa jua husaidia mwili kutokeza vitamini D, kukosa mwangaza wa jua kunaweza kufanya mwili uwe na upungufu wa vitamini hiyo. Hivyo, watu fulani wanapendekeza kwamba watu wale vyakula vingi vyenye vitamini D kama vile, samaki, maini, na vitu vinavyotokana na maziwa.

Mambo yaleyale yanayofanya kuwe na giza wakati wa majira ya baridi kali pia hufanya kuwe na mwangaza mwingi. Dunia inaposonga kwenye mhimili wake, pole kwa pole inageuka na upande wenye baridi unapigwa na jua. Jua huanza kuonekana kwa muda mrefu zaidi katika siku. Kisha kipindi cha kiangazi cha Aktiki huanza. Huo ndio wakati kunapokuwa na mwangaza wa jua hata katikati ya usiku!

[Blabu katika ukurasa wa 27]

Sehemu kubwa ya siku inaweza kulinganishwa na machweo

[Picha katika ukurasa wa 26]

Saa sita mchana wakati wa baridi kali huko Aktiki

[Hisani]

Dr. Hinrich Bäsemann/Naturfoto-Online

[Picha katika ukurasa wa 26]

Watu wengi hufadhaika kwa kukosa mwangaza wa jua