Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mhindi—Mmea wa Ajabu

Mhindi—Mmea wa Ajabu

Mhindi—Mmea wa Ajabu

HADI miaka ya karibuni Harlin alikuwa mkulima wa mahindi katika eneo la Finger Lakes huko New York, Marekani. Yeye hufurahia sana kuwaeleza marafiki na wageni baadhi ya maajabu ya mhindi. Mwandishi wa Amkeni! alimwalika Harlin awaeleze wasomaji wetu baadhi ya mambo anayojua kuhusu mmea huo. Pia tutachunguza mambo mengine kuuhusu. Kwa mfano, mhindi ulitoka wapi? Ulieneaje ulimwenguni pote? Na unatumiwaje? Acheni sasa tuchunguze maelezo ya Harlin kuhusu mmea huo wa ajabu.

Mmea “Unaozungumza” Nawe

“Kwa maoni yangu, mhindi ni mmea wenye utaratibu wa kuvutia. Kuanzia majani yake hadi kwenye mbegu zilizo kwenye hindi lenyewe, kila kitu kimepangwa kwa mpangilio hususa wenye kupendeza. Isitoshe, mmea huu unapokua ‘unazungumza’ nawe. Unakuambia ikiwa una kiu au hauna lishe la kutosha. Kwa kawaida mtoto wa kibinadamu hulia anapohitaji kitu. Kama tu mimea mingine, mhindi hutoa ishara zinazoonekana, kama vile kubadili rangi na umbo la majani yake, ili kueleza mahitaji yake. Unahitaji kuelewa ishara hizo.

“Huenda majani yenye rangi nyekundu ya zambarau yakaonyesha kwamba mhindi hauna fosfati. Dalili nyingine zinaweza kuonyesha ukosefu wa magnesi, nitrojeni, au potashi. Pia, anapouangalia mkulima anaweza kutambua ikiwa mhindi wake una ugonjwa au umeathiriwa na kemikali.

“Kama wakulima wengine wa mahindi, nilipanda baada ya majira ya baridi kali wakati ambapo joto katika udongo huruhusu mbegu ziote. Baada ya miezi minne hadi sita mmea wangu ulipokuwa umekomaa kabisa, kimo chake kilikuwa kama mita mbili hivi.

“Mhindi hukua katika hatua zinazoweza kutambuliwa kwa kuhesabu majani yake. Unapokuwa na majani matano, mmea huo hujichunguzia mahitaji yake. Kwanza, mizizi yake huuchunguza udongo kwa uangalifu na habari inayokusanywa hutumiwa kama msingi wa utaratibu wa ukuzi utakaoamua ukubwa wa bunzi kulingana na idadi ya safu za mbegu. Kisha mmea unapokuwa na majani kati ya 12 na 17, uchunguzi zaidi wa udongo husaidia mmea kuamua idadi kamili ya mbegu katika bunzi. Kwa ufupi, kila mmea huchanganua jinsi ya kupata matokeo bora zaidi kutokana na udongo. Uthibitisho zaidi wa ubuni wake wa ajabu unaonekana katika ustadi wake wa kutokeza mbegu.”

Manyamunyamu, Chavulio, na Nyuzi

“Kila mhindi una sehemu za kiume na za kike. Sehemu ndefu nyembamba inayojitokeza juu ya mmea ndiyo ya kiume, nayo huitwa mnyamunyamu. Kila mnyamunyamu una chavulio 6,000 hivi. Hizo hutokeza mamilioni ya chembe za chavua kwa kila mmea. Chavua hizo hubebwa na upepo hadi kwenye chembe za kike au mayai yaliyo ndani ya mabunzi ambayo hayajakomaa ya mimea iliyo karibu. Mayai hayo hufichwa ndani ya ganda.

“Chavua huingiaje ndani ya ganda na kufikia mayai? Kupitia nyuzi laini nyeupe ambazo huning’inia kutoka kwenye ncha ya bunzi la hindi lililofunikwa kwa maganda. Kila bunzi huwa na mamia ya nyuzi hizo. Ukifuata uzi mmoja hadi chanzo chake utafika kwenye chembe ya kike (ovari), inayobeba yai. Uzi mmoja huwa na yai moja. Kwa hiyo, kila yai hutokeza hindi moja.

“Nyuzi hizo zina nywele laini au stigma ambazo hushika chembe za chavua zinazopeperushwa na upepo. Chembe ya chavua inaposhikwa kwenye sehemu yoyote ya nyuzi, hiyo huota na kutokeza mrija kama mzizi kupitia uzi ili kutungisha yai.

“Ikiwa bunzi halina mahindi yote, hilo linaonyesha kwamba nyuzi fulani hazikuchavushwa, labda kwa sababu hazikukua kwa wakati. Hilo linaweza kusababishwa na udongo mkavu. Kwa kawaida, ikiwa mkulima anajua dalili, anaweza kurekebisha tatizo hilo na kuboresha mazao yake, ikiwa si katika zao hilo labda wakati ujao. Ili kuboresha mazao yangu nilipanda mahindi mwaka mmoja na maharagwe ya soya mwaka mwingine. Maharagwe ya soya ni aina ya mkundekunde unaoongeza nitrojeni katika udongo na viwavi hawawezi kuyaharibu. *

“Mimi hufurahi sana kuona shamba tupu likigeuka polepole na kuwa la kijani na kutokeza chakula kingi sana, bila kelele, uchafuzi, na kwa umaridadi. Ninasadiki kabisa kwamba mihindi, kama tu mimea mingine yote, ni uumbaji wa ajabu. Na bado kuna mambo mengi sana ninayoweza kujifunza kuhusu mmea huo.

Je, maelezo ya Harlin yameamsha upendezi wako juu ya mambo mengine ya mmea huu wa ajabu? Na tuchunguze historia na matumizi mengi ya mmea huo.

Kutoka Mexico hadi Ulimwenguni Pote!

Mhindi ulianza kukuzwa huko Amerika, huenda katika nchi ya Mexico, na kuenea ulimwenguni pote. Waperu walioishi kabla ya enzi ya Wainka waliabudu mungu wa kike wa mahindi aliyepambwa kwa taji lililotengenezwa kwa bunzi za mhindi. Bunzi hizo zilitokea kichwani mwake kama nyaya katika gurudumu. Mwandishi wa vitu vya kiasili Joseph Kastner anaeleza kwamba Wenyeji wa Asili wa Amerika “waliabudu [mahindi] kama kitu kilichotengenezwa na miungu, na kitu ambacho kiliwaumba wanadamu . . . Ilikuwa rahisi sana kuikuza mimea hiyo kwani mhindi mmoja ungeweza kutoa chakula cha kutosha cha mtu mmoja kwa siku moja.” Hata hivyo, wenyeji wa Amerika ya Latini walitumia maharagwe pia na wanaendelea kufanya hivyo hadi leo.

Wakaaji wa Ulaya waligundua mhindi mnamo 1492 baada ya mvumbuzi Christopher Columbus kuwasili katika visiwa vya Karibea. Ferdinand, mwana wa Columbus aliandika kwamba baba yake aliona nafaka “wanayoita mahindi na ina ladha tamu sana ikichemshwa, ikichomwa, au ikisagwa na kuwa unga.” Aliporudi nyumbani, Columbus alibeba mbegu, na “kufikia katikati ya miaka ya 1500,” Kastner anaandika, “[mhindi] ulikua huko Hispania, Bulgaria, na Uturuki. Wafanyabiashara ya watumwa walipeleka mahindi barani Afrika . . . Wafanyakazi wa Magellan [Ferdinand, mvumbuzi Mhispania aliyezaliwa Ureno] waliacha mbegu kutoka Mexico nchini Filipino na Asia.” Mahindi yalikuwa yameanza kutumiwa kwa wingi.

Siku hizi, mhindi ni nafaka ya pili kutumiwa kwa wingi zaidi baada ya ngano. Mchele ni nafaka ya tatu kutumiwa kwa wingi zaidi. Nafaka hizo tatu zinawalisha wanadamu wengi, na pia mifugo.

Kuna aina nyingi za mhindi. Kwa kweli, huko Marekani pekee kuna zaidi ya aina 1,000, kutia ndani mbegu zilizochanganywa. Mimea hukua kufikia kimo cha kati ya sentimita 60 hadi mita 6! Pia urefu wa bunzi hutofautiana. Nyingine zina urefu wa sentimita 5; huku nyingine zikifikia urefu unaostaajabisha wa sentimita 60. Kitabu Latin American Cooking kinasema hivi: “Aina fulani za mhindi unaokuzwa leo huko Amerika ya Kusini, hutokeza bunzi kubwa zilizo na umbo la mpira wa miguu, zenye mahindi yenye urefu wa sentimita 2.5 na upana unaokaribia huo.”

Pia mahindi yanakuwa na rangi tofauti-tofauti. Mbali na manjano, bunzi linaweza kuwa na rangi nyekundu, bluu, pinki, au nyeusi. Nyakati nyingine, mahindi yanaweza kufanya bunzi lionekane kuwa na mistari au madoadoa. Inaeleweka basi kwa nini badala ya kupikwa mara nyingine mahindi yenye rangi tofauti yanatumiwa kutengeneza mapambo.

Nafaka Yenye Matumizi Mengi

Kuna aina nyingi za mahindi zinazogawanywa katika vikundi sita vikuu: dent, flint, flour, sweet, waxy, na popcorn. Mahindi aina ya sweet hayakuzwi sana kama aina nyingine. Utamu unaopatikana katika aina hii ya mahindi unatokana na kasoro fulani ambayo huizuia kubadili kiasi cha kutosha cha sukari kuwa wanga. Zaidi ya asilimia 60 ya mihindi inayokuzwa ulimwenguni hutumiwa kulisha mifugo huku asilimia 20 hivi ikilisha wanadamu. Asilimia inayobaki hutumiwa viwandani au kama mbegu. Bila shaka, matumizi hutofautiana katika nchi mbalimbali.

Mahindi hutumiwa kwa njia mbalimbali. Nafaka hiyo au sehemu yake inaweza kutumiwa kutengeneza vitu mbalimbali kama vile gundi, malai, kileo, au nepi. Hata imetumika katika kutengeneza ethanoli ili kutokeza nishati, ingawa hilo ni jambo linalojadiliwa bado. Kwa kweli, bado mambo kuhusu mmea huu wa ajabu na wenye matumizi mengi yanaendelea kuandikwa.

[Maelezo ya Chini]

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

Mbegu Zilizochanganywa za Mahindi

Katika nchi nyingi, wakulima wa mahindi hutumia mbegu zilizochanganywa kwa sababu zinatokeza mazao mengi. Mbegu zilizochanganywa, hasa za aina ya dent, zinatokezwa kwa kuchavusha kwa uangalifu mimea ya aina tofauti-tofauti na mimea ya aina moja ili kutokeza mbegu bora. Hata hivyo, wanapotumia njia hii wakulima hulazimika kununua mbegu kila mara wanapotaka kupanda. Kwa nini? Mazao ya mbegu zilizochanganywa yanaweza kutofautiana kwa ubora na hayatokezi mazao mengi.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Kuna mahindi ya aina nyingi ulimwenguni pote

[Hisani]

Courtesy Sam Fentress

Courtesy Jenny Mealing/flickr.com