Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mfumo wa ENS (sehemu ya bluu) ndani ya mfumo wa kumeng’enya chakula

Mfumo wa Neva Ulio Tumboni—Je, Ni “Ubongo wa Pili” Katika Mwili Wako?

Mfumo wa Neva Ulio Tumboni—Je, Ni “Ubongo wa Pili” Katika Mwili Wako?

JE, MWILI wako una zaidi ya ubongo mmoja? Ikiwa utajibu “hapana,” uko sahihi. Hata hivyo, kuna mifumo mingine ya neva mwilini. Mfumo mmoja kati ya hiyo unachukua sehemu kubwa sana ya mwili hivi kwamba baadhi ya wanasayansi huuita “ubongo wa pili.” Huo ni mfumo wa neva ambao kwa sehemu kubwa unapatikana tumboni, na unaitwa enteric nervous system (ENS).

Jitihada nyingi zinahitajika na pia sehemu nyingi sana za mwili zinahitaji kuwasiliana ili kuzalisha nishati kutoka kwenye chakula. Kwa hiyo, inafaa sana kwamba badala ya ubongo kusimamia kazi ya kumeng’enya chakula, ENS ndio mfumo unaoongoza kazi hiyo.

Ingawa mfumo wa ENS hauwezi kulinganishwa na ubongo, bado mfumo huo ni tata sana. Katika miili ya wanadamu, mfumo huo una chembe za neva zinazokadiriwa kuwa milioni 200 hadi 600 hivi. Muunganiko tata wa chembe hizo upo ndani ya mfumo wa kumeng’enya chakula. Wanasayansi wanaamini kwamba, ikiwa kazi ya ENS ingefanywa na ubongo, neva ambazo zingehitajika ili kufanya kazi hiyo zingekuwa nene sana. Hivyo, kulingana na kitabu The Second Brain, “ni salama na inafaa zaidi kuacha [mfumo wa kumeng’enya chakula] ujitegemee wenyewe.”

“KARAKANA YA KEMIKALI”

Ili mwili uweze kumeng’enya chakula, kemikali hususa za aina mbalimbali zinapaswa kuzalishwa, kuchanganywa, na kufikishwa eneo husika kwa wakati unaofaa. Profesa Gary Mawe anasema mfumo wa kumeng’enya chakula ni kama “karakana ya kemikali.” Kwa kweli, mchanganyiko huo wa kemikali na jinsi unavyofanywa, ni jambo la kustaajabisha sana. Kwa mfano, katika kingo za utumbo kuna chembe maalumu ambazo hupima aina za kemikali zilizopo kwenye chakula ulichokula. Kisha, habari hiyo hutumiwa na mfumo wa ENS kupanga vimeng’enya vinavyohitajika ili kuvunjavunja chakula katika vipande vinavyoweza kufyonzwa na mwili. Kwa kuongezea, mfumo wa ENS hufanya kazi ya kuhakiki kiwango cha asidi na kemikali zingine kwenye chakula na kuzipatanisha na vimeng’enya vinavyotumika katika kusaga chakula.

Hebu uwazie mfumo wa kumeng’enya chakula kama kiwanda ambacho kwa kiasi kikubwa kinaongozwa na ENS. “Ubongo wako wa pili” hupitisha chakula kwenye mfumo wa kumeng’enya kwa kuchochea misuli iliyo katika kingo za mirija kujibana hatua kwa hatua. Mfumo wa ENS huhakikisha kwamba kiasi cha kubana misuli pamoja na mwendo wake unafaa kabisa kama tu mikanda ya kupitishia bidhaa viwandani inavyofanya kazi.

Mfumo wa ENS husimamia pia suala la usalama. Nyakati nyingine chakula unachokula huenda kikawa na bakteria hatari sana. Haishangazi kwamba asilimia 70 hadi 80 ya chembe za lymphocyte, ambazo ni sehemu muhimu sana ya mfumo wa kinga katika mwili, zinapatikana tumboni! Ikitokea kwamba chakula ulichokula kina bakteria wengi hatari, mfumo wa ENS huulinda mwili kwa kuongeza nguvu na kasi ya kubana misuli ili sumu itoke kwa kutapika au kuharisha.

MAWASILIANO MAZURI

Ingawa huenda ikaonekana kwamba mfumo  wa ENS unajitegemea, bado mfumo huo huwasiliana na ubongo kwa ukawaida. Kwa mfano, mfumo wa ENS unahusika kwenye kazi ya kurekebisha kiwango cha homoni ambazo hupeleka taarifa kwenye ubongo ili kujua kiasi cha chakula unachopaswa kula na wakati wa kufanya hivyo. Unaposhiba, chembe za neva za ENS hupeleka taarifa kwenye ubongo, na huenda zikachochea uhisi kichefuchefu ukila kupita kiasi.

Hata kabla ya kusoma makala hii huenda tayari ulihisi kwamba kuna mawasiliano kati ya mfumo wako wa kumeng’enya chakula na ubongo. Kwa mfano, umewahi kuhisi kwamba kula aina fulani ya vyakula hukufanya ujihisi vizuri zaidi? Utafiti unaonyesha kuwa jambo hilo hutokea ‘taarifa ya furaha’ inapotumwa na mfumo wa ENS kwenda kwenye ubongo na hivyo kufanya uhisi vizuri. Hiyo inatusaidia kuelewa kwa nini baadhi ya watu hula aina fulani ya vyakula wanapokuwa na mkazo. Wanasayansi wanachunguza jinsi wanavyoweza kuchochea utendaji wa mfumo wa ENS ili kutibu ugonjwa wa kushuka moyo.

Mfano mwingine wa mawasiliano kati ya ubongo na mfumo wa kumeng’enya chakula ni kile kinachojulikana kama hisia ya tumbo-joto. Inaelekea hisia hii hutokea wakati ambapo mfumo wa ENS unazuia damu kupita tumboni ubongo unapokuwa na mkazo. Huenda pia mtu akahisi kichefuchefu, kwa sababu wakati wa mkazo ubongo huuchochea mfumo wa ENS kubadili kiasi na mwendo wa kubana misuli ya utumbo. Kulingana na wataalamu, huenda mawasiliano kati ya ubongo na utumbo ndio husababisha mtu ahisi kama tumbo linamwambia afanye uamuzi fulani.

Ingawa mfumo wa ENS unaweza kutokeza hisia zote hizo, hauwezi kufanya kazi ya kufikiri au kuongoza maamuzi yako. Kwa maneno mengine, mfumo wa ENS si ubongo. Hauwezi kukusaidia kutunga wimbo, kufanya hesabu ya pesa ulizonazo benki, au kukufanyia kazi za shule. Hata hivyo, bado wanasayansi wanashangazwa na mfumo huu wa kustaajabisha wenye utendaji tata sana, ambao huenda bado hawajauelewa kikamili. Hivyo basi, kabla ya kula, tulia na ufikirie utendaji unaofanyika katika mfumo wako wa kumeng’enya chakula kama vile usimamizi, uchanganuzi wa habari, ushirikiano wa viungo, na mawasiliano!