Hamia kwenye habari

MACHI 28, 2023
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Kimbunga Freddy Chasababisha Uharibifu Mkubwa Mashariki mwa Afrika

Kimbunga Freddy Chasababisha Uharibifu Mkubwa Mashariki mwa Afrika

Hivi karibuni, eneo la Mashariki mwa Afrika lilipigwa na Kimbunga Freddy, mojawapo ya vimbunga vya kitropiki vilivyodumu kwa muda mrefu zaidi. Kilianza mwanzoni mwa Februari 2023, na kilipiga nchi kadhaa. Kuanzia Februari 21, 2023, kilipiga Madagaska na siku chache baadaye kikavuka mlango wa bahari wa Msumbiji na kuingia Msumbiji na Malawi. Kimbunga hicho kiliendelea kuongezeka na Machi 11, 2023, kikapiga tena Msumbiji. Mikoa mingi nchini Madagaska, Malawi, na Msumbiji imeathiriwa. Katika maeneo haya, upepo wenye nguvu na mvua nyingi zimeleta mafuriko na kuharibu nyumba na kusababisha vifo zaidi ya watu 500 kutia ndani baadhi ya ndugu na dada zetu. Maelfu ya watu wamepoteza makao yao.

Kufikia Machi 27, 2023, hizi ndizo takwimu zilizotufikia. Takwimu hizo zinategemea ripoti za uhakika tulizopata kutoka kwa ndugu walio katika maeneo hayo. Hata hivyo, huenda idadi halisi ikawa kubwa zaidi kwa sababu akina ndugu bado wanatathmini uharibifu uliotokea katika maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi.

Athari Ambazo Ndugu na Dada Zetu Wamepata

Madagaska

  • Wahubiri 256 pamoja na familia zao wamelazimika kuhama makao yao

  • Nyumba 8 ziliharibiwa kabisa

  • Nyumba 29 zilipata uharibifu

  • Majumba 3 ya Ufalme yaliharibiwa

Malawi

  • Inasikitisha kwamba wahubiri 8 walikufa na wengine 6 hawajulikani walipo

  • Wahubiri 3 walijeruhiwa

  • Wahubiri 4,300 hivi pamoja na familia zao wamelazimika kuhama makao yao

  • Nyumba 821 ziliharibiwa kabisa

  • Nyumba 174 zilipata uharibifu

  • Majumba 20 ya Ufalme yaliharibiwa

Msumbiji

  • Inasikitisha kwamba mhubiri 1 alikufa na mwingine 1 hajulikani alipo

  • Wahubiri 880 pamoja na familia zao wamelazimika kuhama makao yao

  • Nyumba 248 ziliharibiwa kabisa

  • Nyumba 185 zilipata uharibifu

  • Majumba 7 ya Ufalme yaliharibiwa

Jitihada za Kutoa Msaada

  • Maeneo mengi yaliyoathiriwa hayawezi kufikiwa kwa sasa

  • Halmashauri za Kutoa Msaada zinaandaa makao, chakula, maji, na bidhaa nyingine muhimu kwa ajili ya wale walioathiriwa

  • Mshiriki wa Halmashauri ya Tawi akifariji kikundi cha ndugu na dada karibu na Chókwè, Msumbiji waliolazimika kuhama makao yao.

    Nchini Msumbiji, kambi ilifunguliwa katika mkoa wa Gaza ili kuandaa makao ya muda kwa ajili ya wahubiri 167 pamoja na familia zao ambao walikimbilia kwenye Jumba la Kusanyiko. Kwa sasa, mamia ya wahubiri wengine wanakaa katika Majumba ya Ufalme na nyumba za watu binafsi katika eneo hilo

  • Nyumba 16 hivi tayari zimerekebishwa

  • Washiriki wa Halmashauri ya Tawi, waangalizi wa mizunguko, na wazee wa maeneo yaliyoathiriwa wanawatembelea watu wa familia mbalimbali ili kujua mahitaji yao na kuwapa faraja

Licha ya hali hizi ngumu, ndugu na dada walioathiriwa bado wanaendelea kufanya mikutano inapowezekana ili kutiana moyo. Tuna uhakika kwamba Yehova atawapa “nguvu zinazopita zile za kawaida” ili wavumilie.​—2 Wakorintho 4:7.