Ona video zinazopatikana

Ona habari zilizo ndani

Jitihada za Kumaliza Umaskini

Jitihada za Kumaliza Umaskini

Jitihada za Kumaliza Umaskini

KWA upande wao, tayari matajiri wamemaliza umaskini. Lakini jitihada za kuwaondolea wanadamu wote umaskini zimeshindwa nyakati zote. Kwa nini? Kwa sababu matajiri kwa ujumla hawataki yeyote au chochote kivuruge utajiri wao. Mfalme Sulemani wa Israeli la kale aliongozwa na roho ya Mungu kuandika: “Tazama! machozi ya wale wanaokandamizwa, lakini hawakuwa na mtu wa kuwafariji; nao wakandamizaji walikuwa na nguvu.”—Mhubiri 4:1.

Je, watu wenye uwezo na mamlaka wanaweza kubadili jamii na kumaliza umaskini duniani? Sulemani aliandika: “Tazama! mambo yote yalikuwa ubatili na kufuatilia upepo. Lililopotoshwa haliwezi kunyooshwa.” (Mhubiri 1:14, 15) Tunaweza kuelewa jambo hilo vizuri kwa kuchunguza jitihada za siku hizi za kumaliza umaskini.

Nadharia za Kumaliza Umaskini kwa Wote

Katika karne ya 19, wakati mataifa kadhaa yalipokuwa yakijikusanyia mali kwa wingi kupitia biashara na viwanda, watu fulani mashuhuri walikuwa wakifikiria hali ya umaskini kwa uzito. Je, maliasili za dunia zingeweza kugawanywa kwa usawa zaidi?

Watu wengine walifikiri kwamba usoshalisti au ukomunisti unaweza kutokeza jamii ya kimataifa yenye usawa, jamii ambayo ingegawanya mali zake kwa usawa. Bila shaka, matajiri hawakupendezwa na jambo hilo. Lakini watu wengi walivutiwa na mwito huu: “Kila mtu anapaswa kuchangia jamii kulingana na uwezo wake, nayo jamii imchangie kulingana na mahitaji yake.” Wengi walikuwa na matumaini kwamba ikiwa mataifa yote yangefuata usoshalisti, ulimwengu ungekuwa mahali panapofaa kabisa kuishi. Mataifa kadhaa tajiri yalianza kufuata sera fulani za usoshalisti na kuanzisha mpango wa kutoa huduma za kijamii bila malipo, yakiahidi kuwasaidia raia zake “kuanzia kuzaliwa mpaka kifo.” Mataifa hayo yanadai kwamba yamemaliza umaskini wa kupindukia miongoni mwa watu wake.

Hata hivyo, usoshalisti haukufaulu hata kidogo kufikia kusudi lake la kuwa na jamii isiyo ya ubinafsi. Lengo la mfumo huo kwamba raia wangefanya kazi ili kuinufaisha jamii badala ya kujinufaisha wenyewe halikutimia. Watu fulani walichukia kuwasaidia maskini, wakisema kwamba ukarimu wao uliwafanya baadhi ya maskini wawe wavivu. Maneno haya ya Biblia yamethibitika kuwa ya kweli: “Hakuna mwanadamu aliye mwadilifu duniani ambaye huendelea kufanya mema na asifanye dhambi. . . . Mungu wa kweli aliwafanya wanadamu wakiwa wanyoofu, lakini wao wenyewe wametafuta mipango mingi.”—Mhubiri 7:20, 29.

Mpango mwingine wa kumaliza umaskini ulipewa jina Ndoto ya Marekani, yaani, ndoto ya kuwa na mahali ambapo kila mtu aliye tayari kufanya kazi kwa bidii anaweza kuwa tajiri. Mataifa mengi ulimwenguni yalianza kufuata sera, kama vile demokrasia na biashara huru, zilizoonekana kuiletea nchi ya Marekani utajiri. Lakini si mataifa yote yaliyofanikiwa kama Marekani kwa sababu bara la Amerika Kaskazini halikupata utajiri wake kutokana tu na mfumo wake wa kisiasa. Bara hilo lilipata utajiri kwa sababu lilikuwa na maliasili nyingi na pia uwezo wa kutumia njia za kibiashara za kimataifa. Zaidi ya hayo, mfumo wa kiuchumi wa ulimwengu wenye ushindani mkali hautokezi tu watu wanaoshinda na kufanikiwa, bali pia wanaoshindwa na kuteseka. Je, mataifa tajiri yanaweza kutiwa moyo yasaidie mataifa maskini?

Mradi wa Marshall —Mbinu ya Kumaliza Umaskini?

Ulaya iliathiriwa sana na Vita vya Pili vya Ulimwengu na watu wengi katika bara hilo wakakabiliwa na njaa. Serikali ya Marekani ilihangaishwa na jinsi nchi za Ulaya zilivyovutiwa na usoshalisti. Hivyo kwa miaka minne, Marekani ilitoa msaada wa pesa nyingi sana ili kufufua viwanda na kilimo katika nchi zilizokubali sera zake. Programu hiyo ya kuzisaidia nchi za Ulaya, iliyoitwa Mradi wa Marshall, ilionekana kuwa na mafanikio. Huko Ulaya Magharibi, uvutano wa Marekani uliongezeka, na umaskini wa kupindukia ukapungua sana. Je, hiyo ndiyo ingekuwa njia ya kumaliza umaskini duniani?

Kufanikiwa kwa Mradi wa Marshall kuliichochea serikali ya Marekani kutoa msaada kwa nchi maskini duniani kote ili kuzisaidia kusitawisha kilimo, huduma za afya, elimu, na usafiri. Marekani ilikubali waziwazi kwamba ilitoa misaada hiyo ili kujifaidi yenyewe. Nchi nyingine pia zilijitahidi kueneza ushawishi wao kwa kutoa misaada. Miaka 60 baadaye, nchi hizo zilikuwa zimetumia pesa nyingi zaidi ya zile Marekani ilitumia katika Mradi wa Marshall, lakini matokeo ya jitihada zao yalikuwa yenye kuvunja moyo. Ni kweli kwamba mataifa fulani yaliyokuwa maskini yalipata utajiri mwingi, hasa huko Asia ya Mashariki. Hata hivyo, ingawa misaada hiyo ilisaidia kupunguza vifo vya watoto na kuwawezesha wengi wao kupata elimu, bado mataifa mengi yaliendelea kupambana na umaskini wa kupindukia.

Kwa Nini Misaada ya Nchi za Nje Haijamaliza Umaskini?

Lilithibitika kuwa jambo gumu zaidi kuyasaidia mataifa maskini kumaliza umaskini kuliko kufufua uchumi wa mataifa tajiri yaliyoathiriwa na vita. Tayari Ulaya ilikuwa na viwanda, biashara, na mfumo wa usafiri. Uchumi wake ulihitaji tu kurekebishwa. Katika nchi maskini, hata misaada ya nchi za nje ilipotumiwa kujenga barabara, shule, na hospitali, watu bado walikuwa maskini wa kupindukia kwa sababu nchi hizo maskini hazikuwa na biashara, maliasili, na uwezo wa kutumia njia za biashara.

Ni vigumu kutatua matatizo yanayosababisha umaskini na yale ambayo umaskini unasababisha. Kwa mfano, magonjwa husababisha umaskini, nao umaskini husababisha magonjwa. Watoto wasipopata lishe bora wanaweza kudhoofika sana kimwili na kiakili hivi kwamba wanapokuwa watu wazima, wanashindwa kutunza watoto wao wenyewe. Pia, nchi tajiri zinapopeleka chakula cha ziada katika nchi maskini kama “msaada,” wakulima na wanaouza bidhaa za kilimo katika nchi hizo hupata hasara, jambo linalosababisha umaskini zaidi. Kutoa msaada wa pesa kwa serikali za nchi maskini kunaweza kutokeza tatizo lingine: Ni rahisi kuiba misaada kama hiyo, na hilo linaweza kutokeza ufisadi, nao ufisadi usababishe umaskini zaidi. Kimsingi, misaada ya nchi za nje hushindwa kumaliza umaskini kwa sababu haiondoi chanzo hasa cha umaskini.

Chanzo cha Umaskini

Umaskini wa kupindukia unatokea kwa sababu mataifa, serikali, na watu mmoja-mmoja wanajitahidi kuendeleza na kulinda faida zao za kibinafsi. Kwa mfano, viongozi wa nchi tajiri hawashughuliki sana na kumaliza umaskini duniani kwa sababu wanachaguliwa kidemokrasia na lazima wawafurahishe watu waliowachagua. Kwa hiyo, wanawazuia wakulima wa nchi maskini wasiuze mazao yao katika nchi tajiri ili kuwalinda wakulima wa nchi hizo tajiri wasipate hasara. Pia, viongozi wa nchi tajiri huwapa wakulima wao msaada mkubwa wa kifedha ili wauze mazao yao kwa faida kubwa zaidi ikilinganishwa na wakulima wa nchi maskini.

Bila shaka, umaskini unasababishwa na mwelekeo wa watu na wa serikali wa kutaka kulinda faida za kibinafsi. Mwandikaji wa Biblia Sulemani alisema hivi: “Mwanadamu amemtawala mwanadamu kwa kumuumiza.”—Mhubiri 8:9.

Kwa hiyo, kuna tumaini lolote kwamba umaskini utaisha? Je, kuna serikali yoyote inayoweza kubadili mwelekeo wa mwanadamu?

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Sheria ya Kukabiliana na Umaskini

Yehova Mungu aliwapa Waisraeli wa kale sheria ambazo kama wangezifuata wengi wao hawangekuwa maskini. Chini ya Sheria, kila familia, isipokuwa kabila la kikuhani la Lawi, ilipokea ardhi kama urithi. Ardhi hiyo ya familia ilikuwa salama kwa kuwa haingeweza kuuzwa milele. Baada ya kila miaka 50, ardhi yote ilipaswa kurudishwa kwa yule aliyeimiliki au kwa familia yake. (Mambo ya Walawi 25:10, 23) Ikiwa mtu angeuza ardhi yake kwa sababu ya ugonjwa, msiba, au uvivu, angerudishiwa ardhi hiyo bila malipo katika mwaka wa Yubile. Hakuna familia ambayo ingelemewa na umaskini miaka nenda miaka rudi.

Pia, kwa huruma Sheria ya Mungu ilimruhusu mtu aliyepatwa na msiba ajiuze kuwa mtumwa. Angepewa mapema pesa ambazo angepata kwa kujiuza ili kulipia madeni yake. Kama hangekuwa amejikomboa kufikia mwaka wa saba, alipaswa kuachiliwa huru na kupewa mifugo na mbegu ili aweze kuanza kilimo tena. Zaidi ya hayo, ikiwa maskini angekopa pesa, Sheria ilikataza kutoza faida. Sheria pia iliwaagiza watu wasivune kingo za mashamba yao ili maskini waweze kuokota masalio. Hivyo, hakuna Mwisraeli angeombaomba.—Kumbukumbu la Torati 15:1-14; Mambo ya Walawi 23:22.

Hata hivyo, historia inaonyesha kwamba Waisraeli fulani walikuwa maskini. Kwa nini? Waisraeli hawakutii Sheria ya Yehova. Kwa hiyo, kama ilivyo katika nchi nyingi, baadhi yao wakawa matajiri waliomiliki ardhi na wengine wakawa maskini wasio na ardhi. Baadhi ya Waisraeli walikuwa maskini kwa sababu watu fulani walipuuza Sheria ya Mungu na kutanguliza faida za kibinafsi tu.—Mathayo 22:37-40.