Hamia kwenye habari

Wanatembea Ndani ya Bahari Kuhubiri Habari Njema

Wanatembea Ndani ya Bahari Kuhubiri Habari Njema

Watu 300 hivi nchini Ujerumani huishi katika visiwa vidogo vya Halligen, vilivyopo kwenye Bahari ya Kaskazini, karibu na pwani ya magharibi ya jimbo la Schleswig-Holstein. Ujumbe wa Biblia huwafikia jinsi gani watu hao?​—Mathayo 24:14.

Mashahidi wa Yehova hutumia feri kufika katika baadhi ya visiwa hivyo vidogo. Hata hivyo, ili kuwafikia watu walio katika visiwa vingine, kikundi kidogo cha Mashahidi hutumia njia tofauti. Wao hutembea kilomita tano hivi kwenye sakafu ya bahari! Hilo linawezekanaje?

Kupwa na Kujaa kwa Maji

Safari zao hutegemea kupwa na kujaa kwa maji. Katika eneo la visiwa hivyo, kimo cha maji ya Bahari ya Kaskazini hupanda au kushuka kwa mita tatu hivi baada ya kila saa sita! Maji yanapokupwa, sehemu kubwa ya sakafu ya bahari huwa bila maji, basi Mashahidi hao wanaweza kutembea ndani ya bahari kufika katika visiwa vitatu vya Halligen.

Safari hiyo hufanywa jinsi gani? Ulrich, mwongozaji mwenye uzoefu anasema hivi: “Tunatumia saa mbili hivi kufika katika visiwa hivyo vya Halligen. Tunatembea bila viatu kwa kuwa ndiyo njia bora ya kuvuka sakafu ya bahari. Wakati wa majira ya baridi tunavaa viatu.”

Mandhari ni tofauti kabisa. Ulrich anasema hivi: “Unahisi kana kwamba unatembea katika sayari nyingine. Sehemu nyingine za sakafu ya bahari ni matope, nyingine zina miamba, na nyingine zimefunikwa na majani. Unaona ndege, kaa, na wanyama wengine wengi.” Pia, mara chache, kikundi hicho cha Mashahidi huvuka vijito vinavyoitwa Priele kwa Kijerumani, ambavyo hufanyizwa kwenye maeneo yenye tope.

Wanaosafiri kwa njia hii hukabili changamoto mbalimbali. Ulrich anaeleza hivi: “Ni rahisi sana kupotea, hasa ukungu unapotanda. Hivyo tunatumia dira na kifaa kinachoongozwa na setilaiti (GPS). Pia, tunahakikisha tunafuata ratiba kabisa ili maji ya bahari yasirudi tukiwa ng’ambo ile nyingine.”

Kuhubiri katika visiwa vya Halligen

Je, bidii hiyo yote imezaa matunda? Ulrich anaeleza hivi kuhusu mwanamume mmoja mwenye miaka 90 na kitu anayesoma kwa ukawaida Mnara wa Mlinzi na Amkeni!: “Siku moja, muda ulituishia hivi kwamba tukashindwa kumtembelea mwanamume huyo. Hata hivyo, kabla tu ya kuondoka katika eneo hilo, mwanamume huyo alitufuata kwa baiskeli na kusema hivi: ‘Je, leo hamtanipa gazeti langu la Mnara wa Mlinzi?’ Kwa kweli, tulifurahi sana kumpatia.”