Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nani Aliyebuni Kwanza?

Ni Nani Aliyebuni Kwanza?

Katika miaka ya karibuni, wanasayansi na wahandisi wamekubali kufundishwa kihalisi na mimea na wanyama. (Ayubu 12:7, 8) Wanachunguza na kuiga maumbile ya viumbe kadhaa—ufundi unaoitwa biomimetics katika lugha ya kitaalamu—wakijaribu kubuni vifaa vipya au kuboresha vifaa vilivyopo. Unapofikiria mifano ifuatayo, jiulize, ‘Ni nani kwa kweli anayestahili kusifiwa kwa ubuni huo?’

Kujifunza Kutokana na Vikono vya Nyangumi

Wanaounda ndege za abiria wanaweza kujifunza nini kutokana na nyangumi mwenye nundu? Mengi. Nyangumi aliyekomaa huwa na uzito wa kilo 30,000 hivi—uzito wa lori lililopakiwa mizigo—naye ana mwili mkakamavu na vikono vikubwa vinavyofanana na mabawa. Inashangaza kwamba mnyama huyo mwenye urefu wa mita 12 husafiri kwa urahisi akiwa majini.

Kilichowashangaza watafiti hasa ni jinsi kiumbe mwenye mwili mkakamavu hivyo anavyoweza kugeuka na kujipinda katika maeneo madogo sana. Waligundua kwamba siri ni umbo la vikono vyake. Upande wa mbele ya vikono vya nyangumi si laini kama bawa la ndege ya abiria, bali umechongoka-chongoka kama meno ya msumeno. Sehemu hizo zilizo kama meno zinaitwa tubercles.

Nyangumi huyo anaposafiri kwa kasi majini, sehemu hizo humsaidia kunyanyuka na kusonga kwa urahisi zaidi pasipo kuzuiliwa na maji. Jinsi gani? Jarida Natural History linasema sehemu hizo hufanya maji yapite kasi na kuzunguka kwa urahisi, hata anapoibuka kutoka majini akiwa wima.10

Ni nani mwenye hataza ya vitu vya asili?

Ugunduzi huo unaweza kutumiwaje? Mabawa ya ndege za abiria yanayoundwa kwa kuiga ubuni huo yatahitaji pindo chache au vifaa vingine vya kiufundi vya kubadili mkondo wa upepo. Mabawa kama hayo ni salama zaidi na rahisi kuyakarabati. Mtaalamu John Long, anaamini kwamba hivi karibuni “kuna uwezekano mkubwa kwamba ndege zote za abiria zitakuwa na vinundu kama vikono vya nyangumi.”11

Kuiga Mabawa ya Shakwe-bahari

Bila shaka, mabawa ya ndege za abiria huundwa kwa kuiga mabawa ya ndege walio hai. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, wahandisi wamepiga hatua katika uigaji wao. Gazeti New Scientist linaripoti hivi: “Watafiti katika Chuo Kikuu cha Florida wameunda ndege ndogo isiyoendeshwa na rubani iliyo na uwezo kama wa shakwe-bahari wa kuumbia hewani, kushuka, na kupaa kwa kasi.”12

Shakwe-bahari hufanya sarakasi zote hizo kwa kukunja na kukunjua mabawa yake kwenye viwiko na mabega. Gazeti hilo linasema kwamba kwa kuiga ubuni huo, “ndege hiyo ndogo yenye ukubwa wa sentimita 60 hutumia mtambo mdogo unaoendesha fito kadhaa za chuma ambazo nazo huendesha mabawa yenyewe.” Mabawa hayo yaliyoundwa kwa ustadi huiwezesha ndege hiyo ndogo kuumbia hewani na kushuka kasi katikati ya majengo marefu. Wanajeshi wana hamu ya kuunda ndege kama hiyo inayoweza kuendeshwa kwa njia za ajabu ili waitumie katika shughuli kama vile kutafuta silaha za kemikali na za kibiolojia katika majiji makubwa.

Kuiga Miguu ya Shakwe-bahari

Shakwe-bahari hagandi kamwe, hata anaposimama kwenye barafu. Kiumbe huyo huhifadhi jinsi gani joto la mwili wake? Siri moja ni maumbile yake ya ajabu ambayo wanyama wengi wanaoishi maeneo yenye baridi kali huwa nayo. Maumbile hayo humwezesha kunururisha joto kinyume cha mkondo.

Uhawilishaji-joto hubaki mwilini. Baridi hubaki miguuni

Unururishaji-joto kinyume cha mkondo ni nini? Ili kuelewa wazo hilo, wazia mabomba mawili ya maji yaliyofungwa pamoja. Bomba moja linapitisha maji ya moto, na lile lingine linapitisha maji baridi. Ikiwa maji ya moto na maji baridi yanatiririka kuelekea upande mmoja, karibu nusu ya joto la maji ya moto litahamia kwenye maji baridi. Lakini, ikiwa maji ya moto na maji baridi yanatiririka kuelekea pande tofauti, karibu joto lote la maji ya moto litahamia kwenye maji baridi.

Shakwe-bahari anaposimama kwenye barafu, vinururishaji-joto kwenye miguu yake hupasha joto damu inaporudi kutoka kwenye miguu baridi ya ndege huyo. Vinururishaji-joto hivyo huhifadhi joto katika mwili wa ndege huyo na kuzuia lisipotee kupitia miguu yake. Arthur P. Fraas, mhandisi wa masuala ya ufundi na usafiri wa ndege, aliufafanua ubuni huo kuwa “mojawapo ya unururishaji-joto unaojifanyiza tena na wenye matokeo zaidi ulimwenguni.”13 Ubuni huo ni wa hali ya juu sana hivi kwamba wanadamu wameuiga.

Ni Nani Anayestahili Kusifiwa?

Sampuli ya gari linaloiga umbo la samaki anayeitwa boxfish ambaye huogelea kwa wepesi sana

Wakati huohuo, shirika la NASA liko katika harakati za kutengeneza roboti yenye miguu mingi inayotembea kama nge, na wahandisi huko Finland tayari wametengeneza trekta lenye miguu sita ambalo linaweza kupanda na kuruka vizuizi kama mdudu mkubwa afanyavyo. Watafiti wengine wamebuni kitambaa chenye pindo ndogo-ndogo zinazoiga jinsi ambavyo koni za msonobari hufunguka na kufungika. Vitambaa hivyo hubadilika kulingana na joto la mwili la mtu aliyevaa vazi lililoshonwa kwa kitambaa hicho. Kiwanda fulani cha magari kiko katika harakati za kutokeza gari jipya linaloiga umbo la samaki anayeitwa box fish ambaye huogelea kwa wepesi. Na watafiti fulani wanachunguza uwezo wa kufyonza mshtuko wa koa za aina fulani ya konokono anayeitwa abalone, wakiwa na lengo la kutengeneza ngao imara zaidi lakini nyepesi.

Uwezo wa pomboo wa kugundua vitu vilivyo majini, unaoitwa sona, hauwezi kamwe kulinganishwa na mashini za mwanadamu za sona

Dhana nyingi nzuri zimetokana na vitu vya asili hivi kwamba watafiti wametayarisha hifadhi ya data ambayo tayari ina maelfu ya mifumo mbalimbali ya kibiolojia. Wanasayansi wanaweza kufanya utafiti kwa kutumia data hizo ili kupata “utatuzi wa asili wanapokumbana na matatizo fulani ya kiufundi,” lasema jarida The Economist. Mifumo ya kiasili iliyo katika hazina hiyo inaitwa hataza za kibiolojia. Kwa kawaida, mwenye hataza ni mtu au kampuni iliyo ya kwanza kuandikisha kisheria wazo jipya au mashine mpya. Likizungumzia hifadhi ya data hizo za hataza za kibiolojia, jarida The Economist linasema: “Wanapourejelea ustadi wa kubuni vitu kwa kuiga vitu vya asili kuwa ‘hataza za kibiolojia’, watafiti hao wanakazia tu kwamba kwa kweli vitu vya asili ndivyo vyenye hataza.”14

Wanasayansi wanachunguza uwezo wa kufyonza mshtuko wa koa za aina fulani ya konokono anayeitwa abalone

Ubuni huo wa ajabu katika vitu vya asili ulitokeaje? Watafiti wengi hudai kwamba ubuni wote huo ulio katika vitu vya asili ulijitokeza wenyewe kupitia mageuzi ambayo yametukia kwa mamilioni ya miaka. Hata hivyo, watafiti wengine wamefikia kauli tofauti. Mwanasayansi Michael J. Behe aliandika hivi katika gazeti The New York Times la Februari 7, 2005: “Ubuni mwingi uliopo [katika vitu vya asili] hutokeza hoja rahisi yenye kusadikisha: ikiwa [kitu fulani] kinafanana, kinatembea, na kulia kama bata, na hakuna ushuhuda wa kuthibitisha vinginevyo, basi lazima tukate kauli kwamba huyo ni bata.” Alimaanisha nini? “Ubuni wa kitu haupaswi kupuuzwa eti kwa sababu tu unaonekana kwa urahisi.”15

Kwa kutumia nguvu za kimolekuli, mjusi anaweza kujitegemeza kwa kujishikilia mahali palipo laini kama uso wa kioo

Bila shaka, mhandisi anayebuni bawa la ndege ya abiria lililo salama zaidi na linalofanya kazi vizuri zaidi anastahili sifa. Vivyo hivyo, mbuni anayevumbua kitambaa laini zaidi, au gari bora zaidi, anastahili sifa kwa sababu ya ubuni wake. Mtu akiunda bidhaa kwa kuiga ubuni wa mtu mwingine na akose kumtaja mbuni mwenyewe, anaweza kushtakiwa.

Sasa fikiria mambo yafuatayo: Watafiti ambao wamebobea katika taaluma zao,wamefanikiwa kwa kiasi kidogo sana kuiga mifumo ya kiasili ili kutatua matatizo ya kihandisi. Hata hivyo, baadhi yao wanadai eti hekima yote iliyo katika vitu vya asili wanavyojitahidi kuiga, haikutokana na chanzo chochote chenye akili, bali ni tokeo la mageuzi. Je, unafikiri dai hilo linapatana na akili? Ikiwa ubuni wenye akili nyingi unahitajika ili kuiga kitu cha asili, basi akili nyingi hata zaidi zinahitajika ili kutokeza kitu hicho cha asili kinachoigwa, sivyo? Kwa kweli, ni nani anayestahili sifa zaidi, mhandisi mkuu au mwanagenzi anayeiga ubuni wa mhandisi?

Kauli Inayopatana na Akili

Baada ya kuona ubuni wa ajabu katika vitu vya asili, watu wengi wanakubaliana na maneno ya mwandikaji wa Biblia Paulo, aliyesema: “Sifa [za Mungu] ambazo hazionekani, zinaonekana waziwazi tangu kuumbwa kwa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zinaeleweka kwa vitu vilivyofanywa, yaani, nguvu zake za milele na Uungu.”—Waroma 1:19, 20.