Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mchongo wa Jiwe Katika Misri ya Kale Unaunga Mkono Simulizi la Biblia

Mchongo wa Jiwe Katika Misri ya Kale Unaunga Mkono Simulizi la Biblia

 Mchongo huo wenye urefu wa mita nane uko karibu na mwingilio wa hekalu la kale la Misri la mungu Amun huko Karnak. Kulingana na wasomi, mchongo huo unaonyesha ushindi wa Farao Shishaki dhidi ya nchi zilizokuwa kaskazini-mashariki ya Misri, kutia ndani Yuda na ufalme wa kaskazini wa Israeli.

Mchongo wa Karnak; picha ndogo inaonyesha watumwa waliofungwa

 Mchongo huo unamwonyesha Amun akimpa Shishaki, au Sheshonk watumwa zaidi ya 150 waliofungwa. a Kila mtumwa anawakilisha mji au taifa moja lililoshindwa. Majina ya miji hiyo imechongwa kwenye mwili wa kila mtumwa. Majina fulani bado yanasomeka, na baadhi yanajulikana vema na wasomaji wa Biblia. Yanatia ndani Beth-sheani, Gibeoni, Megido, na Shunemu.

 Kampeni dhidi ya Yuda inatajwa katika Biblia. (1 Wafalme 14:25, 26) Kwa kweli, Biblia inatoa habari hususa kuhusu uvamizi wa Shishaki. Tunasoma hivi: “Katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu, Mfalme Shishaki wa Misri alishambulia Yerusalemu. . . . Alikuwa na magari 1,200 ya vita, wapanda farasi 60,000, na idadi isiyohesabika ya wanajeshi waliokuja pamoja naye kutoka Misri . . . Aliyateka majiji yenye ngome ya Yuda na mwishowe akafika Yerusalemu.”—2 Mambo ya Nyakati 12:2-4.

 Mchongo huo wa Karnak si uthibitisho pekee wa kiakiolojia kwamba Shishaki alivamia eneo la Israeli. Kipande cha nguzo kilichopatikana katika mji wa Megido wa nyakati za Biblia pia una maandishi yenye jina “Sheshonk.”

 Usahihi wa rekodi ya Biblia kuhusu ushindi wa Shishaki dhidi ya Yuda ni mfano mmoja wa unyoofu wa waandikaji wa Biblia. Waliandika kuhusu ushindi wa taifa lao na pia jinsi lilivyoshindwa. Si kawaida kwa waandishi wengine wa nyakati za kale kuwa wanyoofu kadiri hiyo.

a Matamshi yaliyo katika Biblia “Shishaki” yanaonyesha matamshi ya Kiebrania ya jina hilo.