Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ain Jalut—Vita Vilivyobadili Mkondo wa Historia

Ain Jalut—Vita Vilivyobadili Mkondo wa Historia

Ain Jalut​—Vita Vilivyobadili Mkondo wa Historia

WAPIGANAJI wenye kuogopesha walitoka Mongolia kwa farasi, wakiharibu kila jiji lililokataa kusalimu amri. Katika Februari 1258, waliivamia Baghdad na kupenya kuta zake. Kwa juma zima waliwaua watu na kupora jiji hilo. Nchi zote za Waislamu zilitetemeka kwa hofu kwa sababu ya Wamongolia hao. *

Januari 1260, Wamongolia walisafiri kuelekea upande wa magharibi, na Aleppo, jiji la Siria, likapatwa na hali ileile iliyolipata jiji la Baghdad. Katika mwezi wa Machi, Damasko ilifungua malango yake na kujisalimisha kwa Wamongolia. Muda mfupi baada ya hapo, Wamongolia waliteka majiji ya Palestina ya Nablus (karibu na jiji la kale la Shekemu) na Gaza.

Hülegü, jenerali wa Mongolia, alimwamuru Sultani al-Muzaffar Sayf al-Din Qutuz, aliyekuwa mtawala Mwislamu wa Misri, asalimu amri. Hülegü alimwambia kwamba ikiwa hangefanya hivyo, Misri ingepatwa na hali mbaya sana. Jeshi la Hülegü lilizidi jeshi la Misri la watu 20,000 kwa uwiano wa mwanajeshi 1 kwa 15. “Waislamu walikuwa karibu kutoweka kabisa,” anasema Profesa Nazeer Ahmed, mwanahistoria wa Uislamu. Sultani Qutuz angefanya nini?

Qutuz na Wamamluki

Qutuz alikuwa Mamluki, yaani, mtumwa aliyekuwa na asili ya Kituruki. Wamamluki walikuwa askari-jeshi waliokuwa watumwa wa masultani wa ukoo wa Ayyubid huko Cairo, Misri. Hata hivyo, mnamo 1250, watumwa hao waliwapindua mabwana wao na wakawa watawala wa Misri. Qutuz ambaye pia hapo awali alikuwa askari-jeshi mtumwa, akajinyakulia utawala na kuwa sultani mnamo 1259. Alikuwa mpiganaji stadi na hangekubali kusalimu amri bila kupigana. Hata hivyo, uwezekano wa kuwashinda Wamongolia ulikuwa mdogo sana. Lakini mfuatano fulani wa matukio ulibadili sana mkondo wa historia.

Hülegü aliletewa ujumbe kwamba Möngke, aliyekuwa mtawala mkuu wa Wamongolia, alikuwa amekufa huko Mongolia. Akiona kwamba watu wangeanza kupigania mamlaka huko nyumbani, Hülegü aliondoka pamoja na sehemu kubwa ya jeshi lake. Aliwaacha wanajeshi 10,000 au 20,000 hivi—ambao alidhani kwamba wangetosha kuishinda Misri. Qutuz naye akaona kwamba hali zimebadilika ili kumfaa. Alijiambia kwamba hiyo ndiyo nafasi pekee aliyokuwa nayo ya kuwashinda wavamizi hao.

Hata hivyo, kati ya Misri na Wamongolia kulikuwa na adui mwingine wa Waislamu—majeshi ya wapiganaji wa kidini waliokuwa wameenda Palestina ili kuiteka “Nchi Takatifu” kwa ajili ya dini zilizodai kuwa za Kikristo. Qutuz aliwaomba ruhusa ya kupita na kununua bidhaa kutoka kwao ili apigane na Wamongolia huko Palestina. Wapiganaji hao wa kidini walikubali. Sababu kuu ya kukubali ilikuwa kwamba Qutuz ndiye tu angeweza kuwasaidia kuwaondoa Wamongolia katika eneo hilo, kwani walikuwa tisho kwao sawa na walivyokuwa kwa Waislamu.

Kwa sababu hiyo, uwanja ulikuwa tayari kwa ajili ya vita vya kukata maneno kati ya Wamamluki na Wamongolia.

Ain Jalut Huko Palestina

Majeshi ya Wamamluki na Wamongolia yalikutana Septemba 1260 huko Ain Jalut kwenye Uwanda wa Esdraeloni. Inaaminika kwamba Ain Jalut lilikuwa karibu na jiji la kale la Megido. *

Mwanahistoria Rashid al-Din anasema kwamba Wamamluki waliwavizia Wamongolia huko Megido. Qutuz alificha wengi wa wapanda-farasi wake kwenye milima iliyozunguka uwanda huo na akaelekeza jeshi dogo liwashambulie Wamongolia moja kwa moja ili kuwachochea wawavamie. Wamongolia waliamini kwamba jeshi lote la Wamamluki lilikuwa mbele yao hivyo wakavamia. Kwa ghafula, Qutuz akawashambulia Wamongolia. Aliwaamuru wanajeshi waliosalia watoke walikojificha na kuwavamia Wamongolia kutoka kando. Wamongolia wakashindwa.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Wamongolia kushindwa tangu walipoanza safari kuelekea upande wa magharibi kutoka Mongolia miaka 43 iliyotangulia. Ingawa ni wanajeshi wachache tu waliohusika, inasemekana kwamba vita vya Ain Jalut vilikuwa mojawapo ya vita muhimu zaidi katika historia. Viliwaokoa Waislamu wasiangamizwe, vikakanusha lile wazo la kwamba Wamongolia hawangeweza kushindwa, na vikalisaidia jeshi la Wamamluki kunyakua maeneo yaliyokuwa yametekwa.

Baada ya Vita vya Ain Jalut

Wamongolia walirudi tena mara kadhaa katika eneo la Siria na Palestina, lakini hawakuwahi kushambulia Misri tena. Baadaye wazao wa Hülegü walikuja kuishi huko Uajemi, wakawa Waislamu, na baada ya muda wakawa watetezi wa tamaduni za Kiislamu. Maeneo yao yakaja kujulikana kama maeneo ya Uajemi yanayosimamiwa na mtawala aliye chini ya maliki anayeitwa khan.

Qutuz hakufurahia ushindi wake kwa muda mrefu. Aliuawa na washindani wake muda mfupi baadaye. Kati ya washindani wake kulikuwa na Baybars wa Kwanza, sultani wa kwanza wa ufalme uliounganishwa tena wa Misri na Siria. Wengi walimwona kuwa mtawala aliyeanzisha milki ya Wamamluki. Taifa lake jipya—lililosimamiwa kwa njia nzuri na lenye utajiri—liliendelea kuwapo kwa karne mbili na nusu, hadi mwaka wa 1517.

Katika kipindi hicho cha miaka 250 hivi, Wamamluki waliwaondoa wapiganaji wa kidini kutoka kwenye Nchi Takatifu, wakachochea ukuzi wa biashara na viwanda, wakawategemeza wasanii, na kujenga hospitali, misikiti, na shule. Chini ya utawala wao, Misri ikaja kuwa kituo kikuu zaidi katika ulimwengu wa Waislamu.

Vita vya Ain Jalut viliathiri maeneo mengine mbali na Mashariki ya Kati. Viliathiri pia ustaarabu wa nchi za Ulaya. “Iwapo Wamongolia wangefaulu kuiteka Misri, basi huenda baada ya Hülegü kurudi wangefaulu kupenya kuingia Afrika Kaskazini hadi kwenye Mlango-Bahari wa Gibraltar,” linasema gazeti Saudi Aramco World. Kwa kuwa wakati huo Wamongolia walikuwa pia wamefika Poland, wangeweza kushambulia bara la Ulaya kutoka pande zote.

“Chini ya hali hizo, je, kile kipindi cha Mwamko wa Ulaya kingetokea?” gazeti hilohilo linauliza. “Ulimwengu leo ungekuwa tofauti sana.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Kwa habari zaidi kuhusu Wamongolia na kampeni zao za kivita, ona toleo la Amkeni! la Mei 2008.

^ fu. 11 Kwa sababu vita vingi vya kukata maneno vilipiganwa katika eneo hilo, neno “Megido” likaja kuhusianishwa na vita vinavyojulikana sana vinavyoitwa Har–Magedoni—Har–Magedon katika Kiebrania. Biblia inahusianisha Har–Magedoni na “vita vya ile siku kuu ya Mungu Mweza-Yote.”—Ufunuo 16:14, 16.

[Ramani katika ukurasa wa 12]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Damasko

SIRIA

Ml. Tabori

Uwanda wa Esdraeloni

Ain Jalut (karibu na Megido)

Nablus (Shekemu)

Yerusalemu

Gaza

MISRI

[Picha katika ukurasa wa 12]

Eneo la jiji la kale la Megido

[Picha katika ukurasa wa 13]

Majeshi ya Wamamluki na Wamongolia yalikutana Septemba 1260 huko Ain Jalut kwenye Uwanda wa Esdraeloni

[Hisani ya Picha]

Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.

[Picha katika ukurasa wa 14]

Magofu ya jiji la kale la Shekemu, na sehemu ya jiji la kisasa la Nablus upande wa nyuma