Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Uwezekano wa wanawake wanaoishi katika nchi maskini kufa wakati wa uja-uzito au wanapokuwa wakizaa ni mkubwa zaidi kuliko wa wale wanaoishi katika nchi tajiri.”—BUSINESSWORLD, FILIPINO.

Kulingana na uchunguzi mmoja nchini Ujerumani, asilimia 40 ya watoto kati ya umri wa miaka 11 hadi 15 nchini humo hawajui kwamba jua huchomoza upande wa mashariki; asilimia 60 hawajui kwamba mwezi mpevu huja baada ya kila majuma manne.—WELT ONLINE, UJERUMANI.

Wachimbuaji wa vitu vya kale wamepata hekalu la Wafilisti katika mji wa kale wa Gathi. Jengo hilo linalotegemezwa na nguzo mbili kuu, linatukumbusha simulizi la Biblia kumhusu Samsoni, aliyejishikilia kwenye nguzo kama hizo, na kuliangusha hekalu hilo.—THE JERUSALEM POST, ISRAEL.

Kuoa Wanawake Kutoka Asia

“Wanaume kutoka nchi tajiri za Asia kama vile Japani na Korea Kusini wanatafuta wanawake kutoka nchi maskini [za Asia] kama vile Vietnam na Filipino ili wafunge ndoa nao,” linasema gazeti la Filipino BusinessWorld linalopatikana kwenye Intaneti. Kati ya mwaka wa 1995 na 2006, idadi ya wanaume Wajapani waliooa wanawake kutoka nchi za kigeni iliongezeka kwa asilimia 73. Kwa nini? “Wanawake wanaoweza kujitegemeza hawakubali kuolewa na mtu yeyote tu,” inasema ripoti hiyo, na hawataki sana kuolewa. Kwa upande mwingine, wanawake kutoka nchi maskini zaidi, wako tayari hata kuolewa na wanaume wanaofanya kazi kutoka mataifa tajiri zaidi, kwa sababu wanawapa “tumaini la kuwa na maisha bora.”

Eti Wanaboresha Ukosefu wa Uaminifu?

Kituo cha kuchumbiana kwenye Intaneti kinachozua utata na kinachotoa huduma zake katika nchi tano, kina maneno kwenye nembo yake yanayosema: “Maisha ni mafupi. Anzisha uhusiano nje ya ndoa.” Mwanzilishi wa kituo, anasema kwamba kituo hicho hakiwafanyi watu waache kuwa waaminifu kwa wenzi wao wa ndoa, kwa kuwa wale wanaotumia huduma zao huwa “tayari wameamua kuanzisha uhusiano nje ya ndoa.” “Matatizo mengi yanayotokezwa na ukosefu wa uaminifu hutokea kwa sababu siri ya walio na uhusiano nje ya ndoa hufichuliwa. Tunawapa nafasi watu wanaotaka kuwa na mahusiano nje ya ndoa, wafanye hivyo bila kujulikana,” akasema. “Hatukuanzisha ukosefu wa uaminifu katika ndoa—tumeuboresha tu.” Kwa sasa huduma hiyo inatumiwa na watu milioni 6.4 hivi.

Je, Tumezaliwa Tucheze Dansi?

“Wanadamu wana uwezo wa pekee wa kuongoza viungo vyao vya mwili ili vipatane na mdundo wa muziki, kama vile kuchezesha-chezesha mguu au kucheza dansi,” inasema ripoti iliyochapishwa na watafiti kutoka chuo kikuu cha York, Uingereza, na huko Jyväskylä, Finland. Wachunguzi walisema kwamba hata kabla watoto wachanga hawajaanza kuongea, wao hutambua mdundo wa muziki na kujaribu kusonga kupatana nao. Kadiri wanavyofaulu, ndivyo wanavyotabasamu. Hilo linaonyesha kwamba kutambua mdundo na tamaa ya kusonga kupatana nao si mambo tunayojifunza, bali tunazaliwa nayo.