Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sifongo Hawana Muundo Tata Lakini Wanavutia

Sifongo Hawana Muundo Tata Lakini Wanavutia

Sifongo Hawana Muundo Tata Lakini Wanavutia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

JE, UNGEFURAHIA kuoga kwa mifupa ya mnyama? Huenda hilo si jambo la kupendeza. Hata hivyo, sifongo inayotumiwa kuoga ni mifupa ya nyuzinyuzi ya kiumbe anayeitwa sifongo.

Kulingana na National Geographic News, “sifongo ndio wanyama wa zamani zaidi na wa hali ya chini zaidi kati ya wanyama wote.” Hilo limefanya watu fulani wakisie kwamba wanyama na wanadamu walitokana na sifongo wa zamani. Hata kipindi kimoja cha televisheni kilitaja sifongo kuwa “Hawa wa wanyama,” yaani, “mnyama ambaye alianzisha uhai wote.”

Wanasayansi wamejifunza nini kuhusu sifongo? Je, ni kwamba tu wao ni wanyama wasiokuwa na muundo tata, au wameumbwa kwa njia yenye kuvutia?

Hawana Moyo Wala Ubongo Lakini Hawatatiziki

Huenda sifongo wakaonekana kuwa kama mimea, lakini Aristotle na Plini Mkubwa waliwafafanua kwa usahihi kuwa wanyama. Wataalamu wanakadiria kwamba ulimwenguni pote, kuna angalau jamii 15,000 za sifongo kwenye maziwa na bahari. Jamii hizo zina maumbo na rangi zenye kupendeza. Sifongo wanaweza kuwa na umbo kama la vidole virefu vyembamba, mapipa mapana, mikeka mipana, feni za kifahari, na hata chombo maridadi cha glasi cha kuwekea maua. Wengine ni wadogo kuliko punje ya mchele, na wengine wanaweza kuwa na kimo kinachozidi kile cha mwanadamu. Wanasayansi wanaamini kwamba sifongo fulani wamekuwepo kwa mamia ya miaka.

Kichapo Encyclopædia Britannica kinasema kwamba “sifongo wanatofautiana na wanyama wengine katika muundo, utendaji, na ukuzi.” Jinsi gani? Tofauti na wanyama wengine, sifongo hawana viungo vya ndani. Kwa kuwa hawana moyo, ubongo, au mfumo wa neva, wao huishije? Chembe ndogo sana ndani ya sifongo hufanya kazi nyingi ambazo huendeleza uhai wao. Chembe maalum hukamata chakula, husafirisha virutubisho, au kuondoa uchafu mwilini. Chembe nyingine hutengeneza mifupa au ngozi. Hata chembe nyingine hubadilika na kuwa chembe tofauti kunapokuwa na uhitaji.

Sifongo wa kipekee katika njia nyingine. Ukiponda sifongo katika kichungi, chembe zake zitaungana tena na kufanyiza mnyama yuleyule. Ukisaga sifongo wawili pamoja, chembe zao zitatengana polepole na kuwa tena sifongo walewale. “Hakuna mmea au mnyama mwingine yeyote anayeweza kujifufua kwa njia hiyo,” linasema National Geographic News.

Pia, sifongo huzaana kwa njia ya ajabu. Sifongo fulani hurusha chembe angani ambazo huenea sehemu nyingine na kufanyiza sifongo wengine. Pia, sifongo fulani huzaana kwa kujamiiana, huku wakibadilika na kuwa wa kiume au wa kike uhitaji unapotokea. Sifongo wengine hutaga mayai. “Kadiri tunavyowachunguza zaidi viumbe wasiokuwa na muundo tata, ndivyo tunavyogundua kwamba ni wenye kutatanisha,” anasema mwandishi Paul Morris.

Wasafishaji wa Baharini

Sifongo “hujilisha kwa njia ya pekee kuliko wanyama wengine,” anaandika mtaalamu wa wanyama Allen Collins. Matundu madogo kwenye ngozi huelekeza kwenye vijia na vyumba vinavyopatikana kwenye mwili wote wa sifongo. Kwenye kuta za vijia na vyumba hivyo kuna mamilioni ya chembe ndogo za aina fulani. Kila chembe ina kitu kilichochomoza ambacho husonga mbele na nyuma. Mwandishi Ben Harder anasema hivi: “Kama wapiga-makasia katika meli ya Waroma ya kivita, [chembe hizo] hurusha maji mfululizo kupitia chembe nyingine za sifongo ambazo zimeundwa kwa njia ambayo zinaweza kukamata na kufyonza chakula kutoka kwenye maji.” Sifongo anapopiga maji mara kumi kuliko ukubwa wake kwa saa moja, anatokeza virutubisho, kemikali zenye sumu, na karibu asilimia 90 ya bakteria zote zilizo majini. Sifongo anaweza kudhibiti au kupiga maji kinyume-nyume mkondo wa maji unapobadilika au ili kuondoa uchafu ulio ndani yake. “Sifongo ndio . . . wasafishaji bora kabisa wa baharini,” anasema Dakt. John Hooper.

Uduvi, kaa, na viumbe wengine wadogo hufurahia kuishi ndani ya sifongo kwa sababu ya chakula na maji yanayopita kwa ukawaida ndani yake. Sifongo mmoja alikuwa na wakazi 17,128. Bakteria, mwani, na kuvu wengi hufurahia kushirikiana na sifongo. Bakteria zinaweza kufanyiza asilimia 50 hivi ya uzito wa sifongo mwenye maji.

Wanasayansi wamegundua kwamba sifongo na viumbe wanaoishi ndani yake wanaweza kutokeza dawa mpya na za pekee. Wengine wanaamini kwamba huenda dawa hizo zikasaidia kukabiliana na UKIMWI, kansa, malaria, na magonjwa mengine. Akizungumza kuhusu kitu kilichotolewa ndani ya sifongo, mtafiti Shirley Pomponi anasema hivi: “Tunapata molekuli zenye kupendeza zaidi kutokana na uumbaji kuliko zile zinazoweza kutokezwa na kompyuta.”

Ubuni wa Glasi

Tofauti na sifongo laini na yenye nyuzinyuzi ambayo hutumiwa kuogea, sifongo wengi si laini. Sifongo hao wana mamilioni ya vipande vidogo vinavyofanana na glasi. Vipande hivyo vidogo vinapotazamwa kwa kutumia darubini, vina rangi na maumbo yenye kuvutia sana. Vikiunganishwa katika njia mbalimbali, vipande hivyo vinaweza kutokeza viunzi tata, silaha ya kujikinga, na hata nyaya zenye urefu wa meta 3 hivi na unene wa sentimeta 1. Sifongo mmoja ambaye hula wanyama wengine hutumia nyavu zinazofanana na kroshia [Velcro] kuwinda.

Sifongo anayeitwa Venus flower-basket hutumia vipande vya glasi kufuma wavu unaovutia sana. Nyuzi hizo za silika zinafanana sana na nyaya zilizotengenezwa kwa nyuzi-nyuzi za glasi. Mwanasayansi mmoja anasema, “Nyuzi hizo ni ngumu ajabu. Unaweza kuzikaza kwa nguvu sana lakini hazitakatika kama zile zilizotengenezwa na wanadamu.” Bado wanasayansi hawajaelewa jinsi nyuzi hizo za hali ya juu zinavyotengenezwa katika maji ya bahari na halijoto ya chini sana. Cherry Murray wa Maabara za Bell anasema, “katika kisa hiki, kiumbe asiye na muundo tata anatatua tatizo gumu sana linalokumba teknolojia ya elimu ya nuru na umeme na vifaa vya ujenzi.”

Je, Walijitokeza au Waliumbwa?

Baada ya kuchunguza mambo mengi yenye kuvutia kuhusu sifongo, Hooper anasema: “Kwa kweli, ‘sifongo anayeonekana kuwa hana muundo tata’ ni [mnyama] mwenye kutatanisha, ambaye hadi kufikia leo haeleweki vizuri.” Inafaa kujiuliza hivi: Hali hiyo yenye kutatanisha ilitokeaje na kwa nini? Je, sifongo walijitokeza wenyewe? Au je, mnyama huyo mwenye kutatanisha huthibitisha kwamba kuna Mbuni mwenye akili?

Ingawa huenda watu fulani wakakataa kuchunguza kuwepo kwa Muumba, watu wengi watakubaliana na maoni haya ya mtunga-zaburi wa kale: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza . . . , viumbe hai, vidogo kwa vikubwa.”—Zaburi 104:24, 25.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Muundo halisi wa sifongo. Picha iliyoongezwa ukubwa ya chembe za kurusha maji

[Picha katika ukurasa wa 24]

Vipande vya glasi vya sifongo

[Picha katika ukurasa wa 24]

Venus flower-basket

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Sea horse: Rudie H Kuiter; 3 right-hand inset photos: Dr. John Hooper, Queensland Museum

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Top: Eye of Science/Photo Researchers, Inc.; bottom: Kim Taylor / Warren Photographic