Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Matibabu ya Kisasa Yanaweza Kufaulu?

Je, Matibabu ya Kisasa Yanaweza Kufaulu?

Je, Matibabu ya Kisasa Yanaweza Kufaulu?

WATU wengi hujifunza kutimiza mambo wasiyoweza kwa msaada wa wengine. Jambo sawa na hilo limetukia katika matibabu. Watafiti wa tiba wamefanya maendeleo makubwa kwa kujifunza na kusitawisha matibabu yaliyobuniwa na madaktari na wanatiba maarufu wa kale.

Wanaume mashuhuri kama vile Hippocrates na Pasteur, pamoja na wengine wasiojulikana sana kama Vesalius na William Morton ni baadhi ya madaktari mashuhuri waliokuwapo kale. Wanaume hao waliboreshaje matibabu ya kisasa?

Katika nyakati za kale mara nyingi matibabu hayakutegemea sayansi bali ushirikina na desturi za kidini. Kitabu The Epic of Medicine, kilichohaririwa na Dakt. Felix Marti-Ibañez, chasema hivi: “Ili kupambana na magonjwa . . . , wakazi wa Mesopotamia walitumia imani za kidini katika matibabu, kwa sababu waliamini kwamba magonjwa ni adhabu kutoka kwa miungu.” Matibabu ya Misri yaliyoenea baadaye, pia yalitegemea dini. Kwa hiyo, tangu nyakati za kale, madaktari walisifiwa sana na watu wa dini.

Dakt. Thomas A. Preston asema hivi kwenye kitabu chake The Clay Pedestal: “Imani nyingi za watu wa kale zimeathiri sana matibabu ya leo. Kwa mfano, waliamini kwamba mgonjwa hawezi kuzuia ugonjwa wake. Na kwamba anaweza kutibiwa tu na daktari kwa nguvu za uchawi.”

Kuweka Misingi

Hata hivyo, baada ya muda matibabu yakazidi kuwa ya kisayansi. Hippocrates alikuwa daktari mashuhuri zaidi ya madaktari wote wa sayansi nyakati za kale. Alizaliwa wapata mwaka wa 460 K.W.K., kwenye kisiwa cha Kos huko Ugiriki. Watu wengi humwona kuwa mwanzilishi wa matibabu huko Ulaya. Hippocrates alianzisha matibabu ambayo yalitegemea elimu. Alipinga wazo la kwamba magonjwa yalikuwa adhabu kutoka kwa mungu na kusisitiza kwamba magonjwa husababishwa na hali za asili. Kwa mfano, kwa miaka mingi ugonjwa wa kifafa uliitwa ugonjwa mtakatifu kwa sababu ya imani ya kwamba ungeweza kutibiwa na miungu tu. Lakini Hippocrates akaandika hivi: “Mimi sidhani ule unaoitwa ugonjwa Mtakatifu huletwa na miungu au ni mtakatifu kuliko magonjwa mengine, bali naamini kwamba unasababishwa na hali fulani ya asili.” Hippocrates alikuwa pia daktari wa kwanza kabisa kuchunguza dalili za magonjwa mbalimbali na kuziandika ili zitumiwe baadaye kwa matibabu.

Karne nyingi baadaye, Galen, daktari Mgiriki aliyezaliwa mwaka wa 129 W.K., alifanya pia utafiti wa kisayansi wa hali ya juu. Galen alipasua na kuchunguza miili ya wanadamu na wanyama, kisha akaandika kitabu kuhusu maumbile ya mwili. Kitabu hicho kilitumiwa na madaktari kwa karne nyingi! Andreas Vesalius, aliyezaliwa huko Brussels mnamo mwaka wa 1514, aliandika kitabu On the Structure of the Human Body. Kitabu hicho kilichambuliwa na watu kwa sababu kilipinga mambo mengi yaliyoandikwa na Galen, lakini kiliweka msingi wa elimu ya kisasa ya maumbile ya mwili. Kitabu Die Grossen (Watu Maarufu), chasema kwamba Vesalius alipata kuwa “mmojawapo wa watafiti muhimu sana wa kitiba wasio na kifani.”

Baada ya muda nadharia za Galen kuhusu moyo na mzunguko wa damu zilibadilishwa kabisa. * Daktari Mwingereza William Harvey alipasua na kuchunguza miili ya wanyama na ndege kwa miaka mingi. Alichunguza utendaji wa vali za moyo, akapima kiasi cha damu katika vyumba vyote moyoni, na akakadiria kiasi cha damu mwilini. Mwaka wa 1628, Harvey alichapisha uchunguzi wake katika kitabu On the Motion of the Heart and Blood in Animals. Alichambuliwa, alipingwa, alishambuliwa, na hata kutukanwa. Lakini uchunguzi wake ulileta maendeleo muhimu sana ya kitiba. Aligundua mfumo wa mzunguko wa damu mwilini!

Vinyozi Wanakuwa Wapasuaji

Maendeleo makubwa yalikuwa yakifanywa pia katika upasuaji. Katika Enzi za Kati, nyakati nyingine upasuaji ulifanywa na vinyozi. Si ajabu, watu fulani husema kwamba mwanzilishi wa upasuaji wa kisasa alikuwa Mfaransa aliyeitwa Ambroise Paré aliyeishi katika karne ya 16 na alitumikia wafalme wanne wa Ufaransa. Paré alibuni pia vifaa kadhaa vya upasuaji.

Mojawapo ya matatizo makubwa yaliyowasumbua wapasuaji katika karne ya 19 ni kutoweza kupunguza maumivu wakati wa upasuaji. Lakini katika mwaka wa 1846, daktari wa meno anayeitwa William Morton alianzisha mbinu za unusukaputi katika upasuaji. *

Mnamo mwaka wa 1895, mwanafizikia Mjerumani Wilhelm Röntgen aliona miale ikipenya nyama lakini si mifupa alipokuwa akifanya majaribio kwa kutumia umeme. Hakujua chanzo cha miale hiyo, kwa hiyo akaiita miale x (miale isiyojulikana) au eksirei. Kulingana na kitabu Die Großen Deutschen (Wajerumani Maarufu), Röntgen alimwambia hivi mkewe: “Watu watasema: ‘Röntgen ana kichaa.’” Watu fulani walisema hivyo. Lakini uvumbuzi wake uliboresha upasuaji. Sasa madaktari-wapasuaji wangeweza kuchunguza ndani ya mwili bila upasuaji.

Kushinda Magonjwa

Kwa miaka mingi magonjwa ya kuambukiza kama vile ndui yalienea kasi, yalitisha na kuangamiza watu wengi. Ar-Rāzī, Mwajemi wa karne ya tisa ambaye wakati huo alionwa na baadhi ya watu kuwa daktari mashuhuri zaidi katika nchi za Kiislamu, aliandika ufafanuzi wa kwanza sahihi wa kitiba kuhusu ugonjwa wa ndui. Lakini dawa ya kutibu ndui ilivumbuliwa karne nyingi baadaye na daktari Mwingereza aitwaye Edward Jenner. Jenner alisema kwamba mtu akishikwa na ndui ya ng’ombe (cowpox)—ugonjwa usiodhuru—basi hawezi kuambukizwa ndui (smallpox) tena. Kwa kutegemea uchunguzi huo, Jenner alitumia viini vya ndui ya ng’ombe kutengeneza chanjo ya ndui. Alifanya hivyo mwaka wa 1796. Jenner alichambuliwa na kupingwa kama wavumbuzi wengine waliomtangulia. Lakini hatimaye uvumbuzi huo wa chanjo ulisaidia kukomesha ugonjwa huo na ukatokeza njia mpya ya matibabu.

Mfaransa aitwaye Louis Pasteur alitumia chanjo kupambana na kichaa cha mbwa na maradhi ya mifugo (anthrax). Alithibitisha pia kwamba magonjwa husababishwa na viini. Mwaka wa 1882, Robert Koch aligundua viini vinavyosababisha kifua kikuu. Mwanahistoria mmoja aliuita ugonjwa huo “ugonjwa unaoua watu wengi zaidi katika karne ya kumi na tisa.” Mwaka mmoja hivi baadaye, Koch aligundua viini vinavyosababisha kipindupindu. Gazeti Life lasema hivi: “Kazi ya Pasteur na Koch ilianzisha sayansi ya kuchunguza viini na ikaboresha elimu ya kinga-maradhi, usafi na afya. Uvumbuzi huo umerefusha muda wa maisha ya mwanadamu kuliko maendeleo mengineyo yote ya kisayansi ya muda wa miaka 1,000 iliyopita.”

Matibabu Katika Karne ya Ishirini

Mwanzoni mwa karne ya 20, matibabu yalitegemea mavumbuzi ya matabibu hao wenye akili na wengineo. Tangu hapo, kumekuwa na maendeleo makubwa sana ya kitiba. Wamebuni insulini ya kupambana na ugonjwa wa sukari, tiba ya kemikali kwa ajili ya kansa, homoni za kutibu magonjwa ya tezi, viuavijasumu vinavyotibu kifua kikuu, klorokwini inayotibu aina fulani za malaria na usafishaji wa damu kwa mashine ili kutibu matatizo ya figo, vilevile wamefanya upasuaji wa moyo, na upachikaji wa viungo vya mwili na matibabu mengine mengi.

Lakini sasa tukiwa mwanzoni mwa karne ya 21, je, tiba itaandaa “kiwango kinachokubalika cha afya kwa watu wote ulimwenguni”?

Je, Ni Mradi Usioweza Kutimizwa?

Watu hujifunza kwamba hawawezi kutimiza kila jambo kwa msaada wa wengine. Mambo ya maana sana hayawezi kutimizwa kwa urahisi kila wakati. Vivyo hivyo, tiba imepiga hatua kubwa za maendeleo. Lakini wanatiba wameshindwa kutimiza mradi ulio muhimu zaidi—wa kuandaa afya bora kwa kila mtu.

Kwa hiyo, ingawa katika mwaka wa 1998 Tume ya Ulaya iliripoti kwamba “wakazi wa Ulaya sasa wanaishi kwa muda mrefu wakiwa na afya bora kupita wakati mwingineo wote,” ripoti hiyo iliongezea hivi: “Mtu mmoja kati ya kila watano atakufa kabla ya kufikia umri wa miaka 65. Asilimia 40 hivi ya watu watakufa kutokana na kansa, na asilimia 30 zaidi watakufa kutokana na magonjwa ya moyo . . . Ni lazima watu walindwe na magonjwa mapya.”

Gazeti la Ujerumani la masuala ya afya Gesundheit liliripoti mnamo Novemba 1998 kwamba magonjwa ya kuambukiza kama vile kipindupindu na kifua kikuu yanazidi kuwa hatari. Kwa nini? Viuavijasumu “havina matokeo. Viini vingi haviathiriwi na angalau dawa moja ya kawaida. Na viini vingi sana haviathiriwi na dawa kadhaa.” Magonjwa ya kale yanaibuka tena na magonjwa mapya kama UKIMWI yametokea. Kichapo Statistics ’97 cha Ujerumani kinachozungumzia matibabu chatukumbusha hivi: ‘Hadi sasa, theluthi mbili ya magonjwa yote yajulikanayo—yaani magonjwa 20,000 hivi—hayawezi kutibiwa.’

Je, Matibabu ya Kutumia Chembe za Urithi Ni Suluhisho?

Matibabu mengi ya kisasa yanavumbuliwa. Kwa mfano, wengi huhisi kwamba kurekebisha chembe za urithi kwaweza kuboresha afya. Utafiti uliofanywa nchini Marekani katika miaka ya 1990 na madaktari kama vile Dakt. W. French Anderson, ulisema matibabu ya chembe za urithi ni “njia mpya ya matibabu inayosisimua sana.” Kitabu Heilen mit Genen (Matibabu ya Kutumia Chembe za Urithi) chasema kwamba huenda matibabu ya kutumia chembe za urithi ‘yakawezesha sayansi ya tiba ibuni matibabu muhimu sana. Matibabu hayo yatapambana na magonjwa ambayo hadi leo hayana tiba.’

Wanasayansi wanatarajia kwamba baada ya muda watafaulu kutibu magonjwa ambayo yamerithiwa kwa kuwatia wagonjwa chembe za urithi zilizorekebishwa. Hata chembe zenye kudhuru, kama vile chembe za kansa, huenda zikafanywa ziangamizane. Hivi sasa, mtu anaweza kufanyiwa uchunguzi wa chembe za urithi ili kujua magonjwa yanayomkabili. Watafiti fulani wanasema kwamba mradi utakaofuata ni kupatanisha madawa na maumbile ya chembe za urithi za mgonjwa. Mtafiti mmoja mashuhuri adokeza kwamba siku moja madaktari wataweza “kubaini magonjwa ya wagonjwa wao na kuwatibu kwa kutumia visehemu vya msimbo wa chembe za urithi.”

Hata hivyo, si kila mtu anayesadiki kwamba matibabu ya kutumia chembe za urithi yatatibu magonjwa kimuujiza wakati ujao. Isitoshe, uchunguzi unaonyesha kwamba huenda watu wakakataa kufanyiwa uchunguzi wa maumbile yao ya chembe za urithi. Watu wengi hata wanahofu kwamba matibabu ya chembe za urithi yanaweza kuwadhuru.

Baada ya muda itajulikana kama marekebisho ya chembe za urithi au mbinu nyingine za kisasa za matibabu zitatibu magonjwa kama inavyotarajiwa. Hata hivyo, kuna sababu ya kuwa na shaka. Kitabu The Clay Pedestal chaeleza jambo ambalo hutukia mara nyingi: “Matibabu mapya yanapovumbuliwa, husifiwa sana kwenye mikutano ya kitiba na katika majarida ya kitaaluma. Wavumbuzi wa matibabu hayo hutukuzwa sana, na vyombo vya habari husifu maendeleo hayo. Baada ya msisimko huo wa muda na baada ya watu kuandika manufaa waliyopata kutokana na matibabu hayo ya ajabu, wengi huanza kutamauka hatua kwa hatua, kwa miezi kadhaa au hata miaka kadhaa. Kisha matibabu mengine mapya huvumbuliwa, na kupendwa mno kuliko yale ya awali. Matibabu ya awali hupuuzwa mara moja eti hayafai.” Kwa kweli, matibabu ambayo yanaonwa na madaktari wengi kuwa yasiyofaa yalipendwa sana miaka michache iliyopita.

Ijapokuwa madaktari hawasifiwi na dini kama wale waponyaji wa nyakati za kale, baadhi ya watu huamini kwamba madaktari wana uwezo kama wa miungu, nao huamini kwamba sayansi itatibu magonjwa yote yanayokumba wanadamu. Hata hivyo, jambo la kuhuzunisha ni kwamba sayansi haijafaulu kutibu magonjwa. Dakt. Leonard Hayflick asema hivi katika kitabu chake How and Why We Age: “Katika mwaka wa 1900, asilimia 75 ya watu nchini Marekani walikufa kabla ya kufikia umri wa miaka 65. Leo, hesabu hiyo imebadilika kabisa: asilimia 70 hivi ya watu hufa baada ya umri wa miaka 65.” Ni nini kilichosababisha ongezeko hilo kubwa la muda wa maisha? Hayflick aeleza kwamba hilo “lilisababishwa hasa na kupungua kwa vifo vya watoto wachanga.” Sasa tuseme sayansi ya tiba ingeweza kukomesha hali zinazosababisha vifo vya wazee-wazee—magonjwa ya moyo, kansa, na kiharusi. Je, hilo lingeleta hali ya kutoweza kufa? La hasha. Dakt. Hayflick asema kwamba bado “watu wengi wangeishi hadi umri wa miaka 100 hivi.” Aongezea hivi: “Watu hao wenye umri wa miaka 100 bado hawangekuwa na hali ya kutoweza kufa. Lakini wangekufa kutokana na nini? Wangezidi kudhoofika hadi kifo.”

Licha ya jitihada bora sana zinazofanywa na sayansi ya tiba, matibabu hayawezi kukomesha kifo. Kwa sababu gani? Na je, mradi wa kuandaa afya bora kwa wote ni jambo lisiloweza kutimizwa?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Kitabu The World Book Encyclopedia, chasema kwamba Galen alifikiri kwamba ini lilibadili chakula kilichomeng’enywa kuwa damu. Damu hiyo ilisambaa mwilini na kufyonzwa.

^ fu. 12 Ona makala “Kutoka Maumivu Makali Hadi Unusukaputi,” katika toleo la Amkeni! la Novemba 22, 2000.

[Blabu katika ukurasa wa 4]

“Imani nyingi za watu wa kale zimeathiri sana matibabu ya leo.”—The Clay Pedestal

[Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Hippocrates, Galen, na Vesalius waliweka misingi ya matibabu ya kisasa

[Hisani]

Kisiwa cha Kos, Ugiriki

Courtesy National Library of Medicine

Woodcut by Jan Steven von Kalkar of A. Vesalius, taken from Meyer’s Encyclopedic Lexicon

[Picha katika ukurasa wa 6]

Ambroise Paré alikuwa mwanzilishi wa upasuaji na kinyozi na alitumikia wafalme wanne wa Ufaransa

Daktari Mwajemi Ar-Rāzī (kushoto), na daktari Mwingereza Edward Jenner (kulia)

[Hisani]

Paré na Ar-Rāzī: Courtesy National Library of Medicine

From the book Great Men and Famous Women

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mfaransa Louis Pasteur alithibitisha kwamba magonjwa husababishwa na viini

[Hisani]

© Institut Pasteur

[Picha katika ukurasa wa 8]

Hata kama hali zinazosababisha kifo zingeweza kukomeshwa, bado watu wangekufa kutokana na uzee