Hamia kwenye habari

MSAADA KWA AJILI YA FAMILIA | KULEA WATOTO

Watoto na Simu za Mkononi​—Sehemu ya 2: Kuwafundisha Watoto Kutumia Simu ya Mkononi kwa Busara

Watoto na Simu za Mkononi​—Sehemu ya 2: Kuwafundisha Watoto Kutumia Simu ya Mkononi kwa Busara

 Simu ya mkononi ni kama mashine inayotumia umeme—inaweza kukusaidia au kukudhuru, ikitegemea jinsi inavyotumiwa. Unawezaje kuwafundisha watoto wako kuwa na busara wanapotumia kifaa hicho chenye nguvu? Kwa mfano, utamruhusu mtoto wako atumie simu kwa muda gani kila siku? a

 Unachopaswa kujua

  •   Simu ya mkononi humweka hatarini mtumiaji. Kama ilivyotajwa katika makala “Watoto na Simu za Mkononi—Sehemu ya 1: Je, Mtoto Wangu Anastahili Kuwa na Simu ya Mkononi?” simu ya mkononi inamwezesha mtu kuona kila jambo katika Intaneti, liwe zuri au baya.

     “Ni rahisi kusahau kwamba simu ya mkononi inaweza kuwaonyesha watoto wetu watu na mawazo ambayo ni hatari.”—Brenda.

  •   Watoto wanahitaji mwongozo. Vijana wengi wamezaliwa wakati ambapo teknolojia imeenea sana, lakini watu wazima wengi wameanza kuitumia hivi karibuni tu. Hata hivyo, hilo halimaanishi kwamba wazazi hawajui lolote kuhusu teknolojia na kwamba watoto wanastahili zaidi kuamua ni jinsi gani na ni wakati gani ambapo watatumia simu zao za mkononi.

     Ni kweli kwamba huenda watoto wako wanajua kutumia simu ya mkononi kuliko wewe, hata hivyo, uwezo si ukomavu. Hata watoto wanaojua kutumia teknolojia vizuri bado wanahitaji mwongozo inapohusu kutumia simu ya mkononi kwa busara.

     “Kumpa mtoto wako simu ya mkononi bila kumzoeza ni sawa na kumpa funguo za gari, kumruhusu akae kwenye kiti cha dereva, awashe gari, kisha kumwambia, ‘Tafadhali uwe mwangalifu’ bila kwanza kumfundisha jinsi ya kuendesha gari.”—Seth.

 Unachoweza kufanya

  •   Fahamu programu zilizo katika simu ya mtoto wako. Fahamu programu zitakazomsaidia mtoto wako kutumia simu ya mkononi kwa busara. Kwa mfano:

     Simu yake ina programu gani za kumwezesha mzazi kuzuia matumizi ya mtoto?

     Je, unajua kwamba programu zinazotumiwa kumzuia mtu kutazama mambo yasiyofaa hazitegemeki sikuzote?

     Kadiri unavyojua programu zilizo katika simu ya mtoto wako, ndivyo utakavyokuwa tayari kumsaidia kuitumia kwa busara.

     Kanuni ya Biblia: “Kwa ujuzi mtu huzidisha nguvu zake.”—Methali 24:5.

  •   Weka mipaka. Amua mambo ambayo utaruhusu na ambayo hutaruhusu. Kwa mfano:

     Je, utamruhusu mtoto wako atumie simu wakati wa kula au mnapotembelea familia au marafiki?

     Je, watoto wako wanaruhusiwa kwenda na simu zao usiku kucha chumbani?

     Utawaruhusu watumie programu gani?

     Watumie simu zao kwa muda gani?

     Je, utaweka kiwango cha matumizi ya kila siku?

     Hakikisha kwamba mtoto wako anajua sheria hizo, na uwe tayari kutoa nidhamu mtoto wako anapozivunja.

     Kanuni ya Biblia: “Usimnyime kijana nidhamu.”—Methali 23:13, maelezo ya chini.

  •   Chunguza simu ya mtoto wako. Fahamu nywila ya simu ya mtoto wako, na uangalie mambo anayotazama katika simu yake kadiri inavyohitajika, kutia ndani jumbe fupi, programu, picha, na tovuti alizotembelea.

     “Tulimwambia binti yetu kwamba mara kwa mara tungechunguza simu yake bila kumpa taarifa mapema. Ikiwa tungegundua kwamba ametumia simu yake bila busara, tungemwekea mipaka ya ziada ya matumizi.”—Lorraine.

     Ukiwa mzazi, una haki kabisa ya kujua jinsi simu ya mkononi ya mtoto wako inavyotumiwa.

     Kanuni ya Biblia: “Mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni safi na ya unyoofu.”—Methali 20:11.

  •   Wafundishe watoto wako viwango bora. Msaidie mtoto wako atamani kufanya lililo sawa. Kwa nini hilo ni muhimu?

     Kwa sababu ikiwa mtoto ameazimia kuwaficha wazazi wake jambo fulani, atatafuta njia ya kufanya hivyo licha ya jitihada za wazazi wake kumchunguza. b

    Hivyo, mzoeze mtoto wako kusitawisha sifa bora kama vile unyoofu, kujizuia, na kuwajibika kutokana na matendo yake. Mtoto mwenye viwango bora anaweza kutumia simu yake kwa busara.

     Kanuni ya Biblia: “Watu wakomavu . . . wamezoeza nguvu zao za utambuzi kwa kuzitumia ili kutofautisha mambo yaliyo sawa na mambo yasiyo sawa.”—Waebrania 5:14.

a Katika makala hii, neno “simu ya mkononi” linatumiwa kumaanisha simu iliyo na uwezo wa kuingia kwenye Intaneti. Inafanya kazi sawa na kompyuta ndogo.

b Kwa mfano, vijana fulani hutumia programu zinazoonekana kuwa hazina madhara (ghost) kufunika programu nyingine—kwa mfano, kikokotoo—na hivyo kuficha habari ambazo hawataki wazazi wao wazijue.