Hamia kwenye habari

MACHI 6, 2015
MSUMBIJI

Mashahidi Watoa Msaada Baada ya Mafuriko Nchini Msumbiji

Mashahidi Watoa Msaada Baada ya Mafuriko Nchini Msumbiji

MAPUTO, Msumbiji—Mvua kubwa isivyo kawaida iliyonyesha kuanzia Desemba hadi katikati ya Januari katika jimbo la Zambezia nchini Msumbiji ilitokeza mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu 158. Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Msumbiji inaripoti kwamba hakuna Mashahidi waliokufa au kujeruhiwa. Hata hivyo, mafuriko hayo yaliharibu majengo mawili ya ibada, yanayoitwa Majumba ya Ufalme, na kuharibu nyumba 225 za Mashahidi.

Wajitoleaji Mashahidi wakijiandaa kusafirisha chakula hadi wilaya ya Chire katika jimbo la Zambezia.

Mashahidi walianzisha halmashauri kadhaa za kutoa msaada ili kushughulikia mahitaji ya Mashahidi wenzao katika eneo lililoathiriwa. Majumba fulani ya Ufalme yalitumiwa pia kama makao ya muda na pia kama vituo vya kugawa chakula. Katika eneo la Chire, lililoko kilomita 1,500 hivi kutoka Maputo, mafuriko hayo yaliharibu madaraja ya eneo hilo na hivyo kufanya Mashahidi zaidi ya 1,300 wasiweze kufikiwa kwa barabara. Taasisi ya Usafiri wa Ndege Nchini Msumbiji iliwapa Mashahidi ruhusa ya kutumia helikopta kupeleka zaidi ya tani 17 za misaada katika eneo hilo.

Eneo la Morrumbala, mifuko ya mahindi inashushwa ili watu wagawiwe

Msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Msumbiji, Alberto Libombo, anasema hivi: “Inapendeza sana kuona ukarimu wa Mashahidi wenzetu waliosaidia katika kutoa msaada. Ofisi ya tawi ya Msumbiji inaendelea kupanga jinsi chakula kitakavyowafikia walioathiriwa na pia inapanga jinsi nyumba zao zitakavyojengwa upya au kurekebishwa. Tutaendelea kufanya yote tuwezayo ili kuandaa faraja ya kiroho na msaada ambao waathiriwa wanahitaji.”

Jumba la Ufalme la Chiromo lilitumiwa kama kituo cha muda cha kugawa chakula

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Msumbiji: Alberto Libombo, simu +258 21 450 500